TAARIFA YA MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA
YALIYOFANYIKA KIMKOA KATIKA VIWANJA VYA MNAZI MMOJA,
HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA 16/6/2011
1.0 Utangulizi
Siku ya siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa tarehe 16, Juni ya kila mwaka.
Siku hii inaadhimishwa kwa Azimio la nchi 51 wanachama wa uliokuwa Umoja wa
Nchi huru za Afrika (OAU) kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya kinyama
waliofanyiwa watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini mnamo
mwaka 1976. Hapa nchini kuna utaratibu wa kuazimisha Kitaifa kila baada ya
miaka mitano, mwaka huu maadhimisho yamefanyika Kimkoa. Kwa Mkoa wa Dar
es Salaam maadhimisho haya yalifanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja,
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala. Hii ni kutokana na utaratibu tuliojiwekea wa
kuadhimisha kwa kila mwaka kwa awamu katika Halmashauri za Manispaa za
Mkoa wa Dar es salaam.
2.0 Lengo la Maadhimisho
Siku hii huadhimishwa kwa lengo la kukumbuka mauaji ya kinyama waliofanyiwa
watoto nchini Afrika ya Kusini wakati wakidai haki zao za msingi, pia
kuwakumbusha wazazi/walezi na jamii kwa ujumla juu ya haki na wajibu wa
jamii katika kuwalea watoto. Aidha, hutoa nafasi ya kuwakumbusha watoto haki
na wajibu wao kama watoto katika Taifa.
3.0 Kauli mbiu
Kauli mbiu ya mwaka huu (2011) inasema “Tuungane Pamoja Kuchukua
Hatua za Haraka Kushughulikia Tatizo la Watoto Wanaoishi Mitaani”.
Ikiwa na maana ya kukumbusha umuhimu wa wazazi, walezi wadau wote katika
kushughulikia tatizo la watoto wanaoishi mitaani na kwamba watoto hawa ni
wetu na ndio msingi mkubwa wa kuleta maendeleo ya nchi hii kwa siku za
baadae. Hivyo basi, jamii tunao wajibu kipekee wa kumuandaa mtoto wa taifa
hili ili awe raia mwema.
4.0 Yaliyojitokeza
• Risala ya watoto
• Hotuba ya Mgeni rasmi
• Vikundi vya burudani
• Mgeni rasmi kutembelea mabanda
4.1 Risala ya watoto
Watoto walipata nafasi ya kusoma risala mbele ya Mgeni rasmi, wazazi, walezi na
wadau mbalimbali ambayo iliwasilishwa kwa niaba ya watoto wenzao wa Mkoa
wa Dar es salaam. Katika risala yao watoto walimshukuru mgeni rasmi kwa
kukubali kuungana nao katika maadhimisho hayo. Risala hiyo ilitoa ujumbe
mbalimbali ikiwa ni pamoja na;-
Jamii kuweka utaratibu wa kuwahudumia watoto wote bila kubagua
•
Serikali iangalie namna ya kuondoa umaskini wa kipato katika ngazi ya
•
familia
Baadhi ya watu katika jamii waache tamaa ya kuchukua mali na kuwaacha
•
watoto wakihangaika mitaani pindi wazazi wao wanapofariki dunia.
Pia, risala ilibainisha vyanzo vya watoto kwenda kuishi mitaani kama vile,
kutopata upendo kutoka kwa wazazi na walezi, matatizo mimba za utotoni, utoro
shuleni na tamaa. Hivyo jamii na watoto wanapaswa wafahamu haki na wajibu
wao.
4.2 Hotuba ya Mgeni rasmi
Hotuba ya Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Said Meck
Sadick katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ilisomwa na Ndugu E.
Ntandu Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Mipango na Uratibu aliyemwakilisha
Kaimu Mkuu wa Mkoa katika maadhimisho hayo. Katika hotuba yake Mgeni rasmi
aliwashukuru Wataalamu wa Sekretarieti na Halmashauri za Manispaa katika
kuandaa siku hiyo. Aidha, alitoa Shukrani za dhati kwa Shirika la AMREF, Benki
ya CRDB, Benki ya Wananchi, Shirika lisilo la kiserikali la Dar Urban Plan na
Wadau wengine wote kwa kutambua mchango wao katika kuadhimisha siku ya
Mtoto wa Afrika ndani ya Mkoa wetu. Pia alisisitiza kwamba kwa mwaka ujao
wazazi na walezi wengi wahamasishwe ili waungane pamoja na watoto wao
katika kuadhimisha siku hiyo ili ujumbe unapotolewa uweze kuwafikia.
Mgeni rasmi alitoa wito kwa jamii itimize wajibu wake kama kauli mbiu ya
mwaka huu unavyotutaka na kuahidi kwamba Mkoa utaendelea kutoa fursa kwa
watoto ili kuweza kutoa maoni yao kwa Maendeleo ya Taifa na kuwachukua
hatua kali za kisheria wale wote wanaoendeleza ukatili dhidi ya watoto.
Vikundi vya burudani.
4.3
Watoto walipata nafasi ya kuonesha burudani mbalimbali kwa Mgeni rasmi na
watu wote waliofika katika viwanja vya Mnazi Mmoja. Burudani hizo zilikuwa ni
pamoja na Ngoma ya mganda, kwaya na maigizo zikiwa zimebeba ujumbe
mbalimbali kama vile, ajira za watoto zikomeshwe na wazazi na walezi
wapelekwe watoto shuleni kwani uridhi pekee wa wazazi kwa watoto ni elimu,
jamii iwalee na kuwatunza watoto. Aidha, Serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii
juu ya haki na wajibu wa watoto na jamii.
4.4 Mgeni rasmi kutembelea mabanda
Mgeni rasmi alipata nafasi ya kutembelea mabanda ambayo yalishehenezwa na
kazi mbalimbali za watoto zikiwemo; - picha za kuchora, vifaa vya kufinyanga
kwa udongo (kinu na kibao cha kusukumia chapati), bangili za wanawake za
kuvaa mikononi ambazo hutengenezwa na watoto wenye ulemavu wa macho.
5 Hitimisho
Kila mmoja wetu awajibike kwa nafasi aliyonayo katika kuhakikisha tatizo la
watoto wanaoishi mitaani linatoweka na hatimaye kuwa na Taifa endelevu lenye
kutekeleza na kusimamia misingi ya haki na wajibu kwa watoto.
No comments:
Post a Comment