NGUVU YA HABARI

Thursday, December 27, 2012

Kwa nini watanzania waitwe masikini wakati kuna malighafi za kutosha?


Tanzania bara ilipata uhuru mwaka 1961 kutoka mikononi mwa Waingereza, chini ya mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa Waziri Mkuu wa Kwanza. Mwalimu Nyerere aliposhika tu madaraka alitangaza vita dhidi ya  maadui watatu Maladhi, Ujinga na Umasikini ambao maadui hawa walionekana kuwanyanyasa Watanzania.
Kwa kutambua umuhimu wa kupambana na maadui hawa, Mwalimu Nyerere akishirikiana na viongozi wenzake kupanga sera mathubuti za kutokomeza maadui hao.

Kutoa elimu bure kwa watanzania hususani vijana, kuboresha miundo mbinu pamoja na kuboresha huduma muhimu za jamii yaani vituo vya afya na hospitali ni mbinu moja wapo aliyotumia kupigana na maadui hao.

Aidha, alitangaza Azimio la Arusha 1967 iliyoanisha maadili ya viongozi na kujali usawa kwa watanzania wote bila kuweka matabaka ya wenye nacho na wasio nacho yaani mfumo wa Ujamaa.

Ingawa miaka ya 1970 hadi 1980 Tanzania ilianza kuyumba katika mapambano dhidi ya umasiki huku adui ujinga akionekana kupunguzwa kasi.

Mwalimu Nyerere mwaka 1985 aliamua kumwachia madaraka Mzee ruksa, Ali Hassan Mwinyi, ambaye naye alipambana vilivyo na maadui hao, na kumwachia Rais mstaafu Benjamin Wilium Mkapa.
Rais Mstaafu wa Tanzania,Ali Hassan Mwinyi
Mkapa alikuja na sera ya uwekezaji binafsi (Ubinafsishaji) katika harakati za kupambana na maadui hao, ingawa hakutoa matokeo ya mapambanao hayo na kumwachia Rais Jakaya Kikwete ambayo naye anasubiriwa kutoa matokeo ya mapambano hayo.

Kumbuka silaha kubwa ambayo watanzania wanajivunia kuwashinda maadui hao ni kutokana na kumiliki rasilimali nyingi ambazo ni jibu tosha la kuwashinda maadui hao.

Adui umasikini anatokomezwa kwa kutumia vizuri rasimali zilizopo ambazo baadhi ya rasilimali hizo hazipatika nchi nyingine yo yote.

Adui Ujinga anatokomezwa kwa kuboresha tasnia ya elimu ambayo ndiyo ukombozi na silaha kuu ya kumuua adui huyo.

Adui huyu ujinga hawezi kutokomezwa kama tasnia ya elimu haina fedha za kutosha ili kuboresha miundo mbinu pamoja na mishahara ya walimu na wadau wengine wa elimu.

Wakati huo huo, kitega uchumi cha fedha zitakazosaidia kuwaua maadui ni rasilimali zilizopo nchi Tanzania na sio misaada ya nje, kwa maana ‘fimbo ya mbali haiui nyoka’ na ‘Mtegemea cha nduguye hufa angali masikini’.

Tanzania kama nchi nyingi tangu itangaze vita dhidi ya maadui hawa ni takribani miaka 51 imepita, huku jamii ikisubiri kutawazwa ubingwa dhidi ya maadui hao.

Cha kushangaza wakati Tanzania Bara ikisherekea miaka 51 ya uhuru, serikali ilikiri kushindwa kutokomeza maadui hao hususani Umasiki huku ikiwa imekalia silaha za kutosha kumshinda adui huyo, ama kweli ‘kwenye miti mingi hakuna wajenzi’ na ‘upele humwota asiye na kucha’.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, katika mdahalo wa uhuru ulioandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) kwa kushirikiana na ITV na Capital Radio, alikaririwa  alisema ni kweli Tanzania ni masikini na wasomi hawana budi kushirikiana na serikali kutafuta njia za kutokomeza umasikini nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Serikali imetangaza vita nyingi dhidi ya adui umasikini ikisahau kuwa vita ilikwisha tangazwa na Mwalimu Nyerere tangu miaka ya 1967 na kinachosubiriwa ni kutangaza matokeo ya ushindi ama kushindwa.

Je, ni kweli Tanzania ni nchi masikini kama inavyo daiwa na serikali? Ukizingati Tanzania ina mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro na vivutio vya kihistoria kama Bagamoyo, Kalenga na Lugalo (Iringa) ambako haya ni baadhi ya vivutio vya watalii vinavyo iingizia nchi fedha za kigeni.

Umasikini unatoka wapi Tanzania kama Tanzania ina maziwa, bahari, ardhi nzuri kwa kilimo cha mazao na ufugaji?

Je, miaka 51 ya uhuru wa Tanzania bara, elimu inayotolewa vyuoni haiwaandaa wanafunzi kujitegemea na kuisaidia nchi kuikomboa mikononi mwa maadui hao?

Kwa upande wa wasomi wanachuliaje kauli hii ya serikali kusema Tanzania ni nchi masikini?

Prof. Issa Shivji anapingana na kauli ya serikali kwa kuainisha vitega uchumi ambavyo Tanzania inamiliki kama vile madini, na mbuga za wanyama.

Prof. Shivji amedai kuwa Tanzania si masikini ila tatizo linalofanya watanzania waonekana masikini ni serikali kuunda sera thabiti inayosimamia masilahi ya wananchi wa Tanzania na hatimaye imejikuta ikitetea masilahi ya wawekezaji wa kigeni.

Prof. Shivji amesema wachimbaji wa madini wazawa hawawezeshwi na serikali na hatimaye wanapochimba madini huitwa wamefamia madini ya wawekezaji na kuitwa wavamizi.

Mhadhiri wa Kiswahili katika chuo Cha Dar es Salaam, Dr. Martha Qorro anadaiwa kuwa Tanzania ina rasilimali za kutosha ambazo zikitumiwa vema zitawakomboa Watanzania,

Dk. Qorro anadai kuwa watanzania wanashindwa kutumia rasilimali ziulizopo kutokana na serikali kutokuwa na sera inayoeleweka kuwa Lusha ipi itimike kufundishia elimu ya msingi ha vyuo vikuu ili kuwaandaa vizuri wananchi kutumia rasilimali zao kwa manufaa ya Watanzania.

Amesema lugha ya Kiingereza inayotumika kufundishia elimu ya sekondari na vyuo vya kati na vyuo vikuu haimsaidii mwanafunzi kumuuandaa kuja kutumia rasilimali zilizopo kwa sababu ni lugha ya Kigeni na Watanzania walio wengi hawaijui lugha hiyo.

Dr.Qorro napendekeza Lugha ya Kiswahili itumike kufundishia tasnia ya elimu katika nyanja zote ilikumuandaa mwanafunzi aje atoe mchango mkuu wa kutumia rasilimali zilizopo.

Aidha, mwanasiasa wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Esther Wasira, anakanusha Tanzania si nchi masikini kama inavyodaiwa na serikari, kwa kuwa ina rasilimali nyingi ambazo zinaweza kumkomboa mtanzania.

Wasira anaona kinachochangia watanzania waonekane ni masikini ni serikali kushindwa kutokomeza rushwa inayofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali na wafanyabiashara.

Amesema serikali imekuwa mtazamiji wa vitendo vya rushwa na kushindwa kuchukua hatua mahususi dhidi ya wahujumu uchumi hao.

Akitolea mfano wa chaguzi za chama tawala (CCM), ambazo mwenyekiti wa taifa wa chama tawala, Jakaya Mrisho Kikwete alikiri akikithiri kutendeka kwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa wanawake na hakuna hatua yo yote ambayo imefanyika licha ya Mwenyekiti kutambua vitendo hivyo.

Anaongeza kuwa serikali kushindwa kuwachulia hatua watuhumiwa wa EPA na RICHMOND ni dhahiri ina bariki umasikini uendelee kuwameza watanzania, na kuwanufaisha wahujumu uchumi wan chi.

Aidha, Wasira anaona kukosekana kwa maadili na miiko kwa viongozi ndiko kunako changia umasikini nchini kwa sababu viongozi hawa  wanatanguliza masilahi ya watu wachache.

Watanzania wana nafasi kubwa ya kutokomeza umasikini iwapo watatunga sheria ya wazi ya kuwabana viongozi kwa kuwahoji pindi wanaposhindwa kutekeleza ahadi na kuvuja mali za umma, na kuwachagua viongozi waadilifu ambao wapo tayari kuutumikia umma kwa kutetea masilahi ya watanzania na sio wawekezaji wa kigeni na watu wachache.

No comments: