NGUVU YA HABARI

Friday, January 17, 2014

Kiza cha Tandaa Uhuru wa Vyombo vya Habari Tanzania

TAKRIBANI miaka hamsini na miwili imepita toka Tanzania Bara ipate Uhuru wa kisiasa. Watanzania wengi wamekuwa wakifurahia Uhuru huo huku waandishi wa Habari wakiendelea na harakati za kutafuta Uhuru wa vyombo vya habari licha ya wakoloni kuwaachia Uhuru wa kisiasa watanzania toka mwaka 1961 Disemba 9.
Kutoka na kukosekana kwa Uhuru wa vyombo vya Habari nchini, watanzania wameshuhudia kufungiwa kwa vyombo vya Habari kama vile kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi mwaka 2008 miezi mitatu, na Julai 30 mwaka 2012 limefungiwa kwa muda usiofahamika, kuuawa kwa mwandishi wa Habari Daud Mwangosi, na kutekwa na kuteswa kwa Absalum Kibanda, kutishiwa kwa waandishi wa habari.


Waandishi wa habari wakiwa katika harakati za kuhakikisha wanapata picha za chanzo chao cha habari na baadaye kuandaa habari hiyo kwa manufaa ya msikilizaji au mtazamaji.


Maandamano ya Waandishi wa habari wa Nigeria wakipinga ukandamiza wa uhuru wa vyombo vya habari nchini humo.

Waandishi wa habari wakiendeleza maandamano ya kupinga mauaji kwa waandishi wa habari yanayodaiwa kufanywa na vyombo vya usalama wa raia. (Picha imechukuliwa Mtandaoni)

Kilio cha waandishi wa Habari Tanzania ni matokeo yaliyosababishwa na serikali ya wazawa kurithi sheria iliyotungwa na Bunge la serikali ya kikoloni la Tanganyika ambalo liliundwa mwaka 1926 na mwaka 1928, bunge hilo la Tanganyika lilitunga Sheria ya Magazeti Na. 22 ya mwaka 1928 kuzuia machapisho yoyote yaliyokuwa yakipinga utawala wa serikali ya kikoloni na kuwataka wananchi wawaunge mkono wanaharakati wa Uhuru.
 Serikali ya kikoloni ya Waingereza ilitunga sharia hiyo ilikudhibiti makundi ya wanaharakati waliokuwa wakitumia vyombo vya Habari kupinga na kukosoa utawala wa kikoloni na ambao pia walikuwa wakipigania Uhuru wa mwaafrika kujitawala mwenyewe.
Aidha, Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) Dk. Ayub Rioba katika kitabu chake cha ‘Historia ya Vyombo vya Habari Tanzania’ (The Media History of Tanzania) aliandika kuwa mwaka 1952 Agosti Bunge la Tanganyika lilikaa kikao na kufanyia marekebisho ya Sheria ya Magazeti Na. 35 ya 1952 ambapo vifungu vya jinai  za kashfa na uchochezi vilipitishwa na bunge hilo na lilipendekeza adhabu kwa mwandishi wa Habari atakayekiuka vifungo hivyo kulipa faini ya Dola za Marekani $ 400 hadi $ 1300.
Muathirika wa kwanza wa sharia hiyo alikuwa Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tanganyika African Nation Union (TANU) pamoja na wenzake walikamatwa kwa madai waliandika Habari za uchochezi.
Kukamatwa kwa Mwalimu Nyerere na wenzake kulichochea zaidi waandishi wa Habari kuichukia serikali hiyo kwa madai inatumia sheria kandamizi kuzuia harakati za ukombozi wa Mtanzania kutoka mikononi mwa Waingereza.
Kila lililo na mwanzo halikusikuwa na mwisho, hatimaye Tanganyika ikapata Uhuru wake Disemba 9, mwaaka 1961, na Zanzibar kufanya Mapinduzi tarehe 12 Januari 1964 na kisha mwaka 1964, Aprili 26, Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hali hiyo ilidhaniwa ingepoteza machungu ya waandishi wa Habari kunyanyaswa na wakoloni.
Pema ukipema si pema tena, baada ya Muungano wa za Tanganyika na Zanzibar Uhuru mwandishi wa Habari ukabaki kitendawaili pale Serikali ya wazawa iliyokuwa ikitumia magazeti na redio kuhubiri harakati za ukombozi wa mwafrika na ujenzi wa taifa jipya mwaka 1976 ikatunga sheria ya Magazeti Namba 3 na kusainiwa na Rais Mwalimu Nyerere April 3, 1976 ambayo ikaendeleza kiama cha kumnyimwa uhuru mwaandsishi wa Habari na kumfanya aendelee kukumbuka machungu ya wakoloni.
Aidha, sheria hiyo iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo sheria iliyokuwa ikipingwa vikali na wanaharaki hao wakati wa kupigania Uhuru wa mwaafrika kipindi cha ukoloni na baada ya kupata Uhuru sheria hiyo ilirithiwa tena bila kujali kama ni sheria ile ile iliyomweka hatiani Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Mbali ya sharia hiyo kandamizi ya Magazeti ya mwaka 1976, mwandishi wa Habari amejikuta akishindwa kufanya kazi ya kuutumikia umma kupitia vyombo vya Habari kutokana na kuwepo pia sheria nyingine zinazombana.
Sheria ya Usalama wa Taifa (National Security Act No. 6 of 1970) iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungana 19 Machi 1970 ni mojawapo ya sheria zinazobinya Uhuru wa mwandishi wa Habari kwa kuzuia mambo ambayo yanadaiwa kuwa nyaraka za siri za taifa amabazo hazitakiwi kuandikwa. Lakini nyaraka hizo hazijakuwekwa bayana zipi ni nyaraka za siri na zipi si nyaraka za siri hasa kipindi hiki ambacho serikali inasisitiza utawala bora na uwazi.
Wakati wa waandishi wa Habari wakitafuta namna ya kujikomboa mikononi mwa adui wao wa Uhuru wa vyombo vya Habari, kiza kilizidi kutawala kwa wanahabari na wadau wa Habari pale serikali ilipopeleka muswada wa marekebisho ya sheria ya habari bungeni ikiwa imejaa vipengee vinavyozidi kuwakandamiza waandishi wa habari na vyombo vya Habari kwa kupendekeza adhabu ya sh milioni tano au kifungo cha miaka mitano au vyote kwa pamoja.
Hata hivyo muswada huo wa marekebisho ya sheria ya magazeti ya mwaka 1976 sura ya 229 Bunge uliyokuwa na lengo la kuwatia kitanzi waandishi wa habari na vyombo vya Habari vitakavyochapisha habari zilizodaiwa za uvunjivu wa amani au uchochezi ulipingwa bungeni Novemba 8 mwaka jana na huku wabunge wengi waliitaka serikali kufanya mabadiliko kamili ya sheria ya habari.
Kilio cha waandishi wa Habari kilioneka kuungwa mkono pale spika wa Bunge Anne Simamba Makinda aliposema anaishangaa serikali kuona ikiendelea kuweka viraka vya sheria ya magazeti badala ya kuipeleka bungeni ifanyiwe mabadiliko yote.
“Tumefanya utani katika sheria hii kwa muda mrefu, sitaki utani. Serikali leteni muswada wa sharia ya Habari,” alisisitiza Spika wa Bunge Makinda.
 Kuendelea kutumia sheria zinazoingilia Uhuru wa vyombo vya Habari ni sawa na kuenzi utawala wa kikoloni ambalo ulitunga sheria za kubinya Uhuru wa vyombo vya Habari katika kuikosoa serikali ili kuzidi kuwapumbaza wananchi wasitambue kama wanaibiwa haki na maliasili zao, wananyonywa, wananyanyaswa na kubaguliwa na serikali ya kikoloni.
Aidha, kuwepo kwa sheria zinazonyima Uhuru wa waandishi wa Habari zinachangia pia kurudisha nyuma Maendeleo ya nchi kwa kuwa Uhuru huendana na Maendeleo.

Waandishi wa habari wakimsikiliza Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe akitolea ufafanuzi wa kuvuliwa nyadhifa zake na kamati kuu ya CHADEMA kwa tuhuma za kukihujumu CHADEMA
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika kitabu chake cha ‘Uhuru na Maendeleo’ alisema; “Uhuru na Maendeleo ni vitu vinavyohusiana sana; uhusiano wao ni sawa na uhusiano baina ya kuku na yai! Bila kuku hupati mayai; na bila mayai kuku watakwisha. Vilevile bila ya Uhuru hupati Maendeleo, na bila ya Maendeleo ni dhahiri Kwamba Uhuru wako utapotea.”
Ili Tanzania itimize azma ya kuwa na maendeleo ya uchumi, kisiasa na kijamii inahitaji kufanya mabadiliko makubwa katika sheria zinazonyima Uhuru wa mwandishi wa Habari ili kutoa fursa kwa waandishi wa Habari kufanya Habari za uchunguzi na upembuzi yakinifu ambao pia utasaidia kuwaunganisha wananchi na serikali yao katika kupanga na kutekeleza mambo yanayowahusu.
Vilevile kuwapa Uhuru waandishi wa Habari kwa kuondoa sheria kandamizi kutawapa nafasi waandishi wa Habari kufichua mambo mbalimbali ambayo ni kikwazo cha maandeleo ukiwemo ufisadi rushwa na mikataba ya ulaghai inayoiingizia hasara taifa.
Kutokana na kuwepo kwa nyaraka nyingi za siri kulipelekea gazeti la Mwananchi kufungiwa wiki mbili baada ya kuchapisha taarifa za mishahara ya watumishi wa umma ambayo wanalipwa na kutokana na kodi ya wananchi.
Baba wa taifa katika kitabu chake cha ‘Uhuru na Maendeleo alisema, “Utumiaji wa nguvu, na kutoa ahadi za uwongo, mambo hayo yanaweza kuleta mafanikio kwa muda mfupi tu. Hayawezi kuleta nguvu kwa taifa au kijiji, wala hayawezi kuweka msingi wa Uhuru wa watu, au usalama wa mtu binafsi au wa kikundi cha watu.
Iwapo serikali itasikia kilio cha waandishi wa Habari wanaopinga sheria kandamizi basi mchango wa vyombo vya Habari katika Maendeleo ya nchi utaonekana kwa uwazi.

Toka sheria ya Magazeti itungwe mwaka 1976 na kusaini na Baba  wa taifa na rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Nyerere tarehe 3, Aprili 1976 ni takribani miaka 38 imepita serikali haijawahi kupeleka muswada wa Habari bungeni.


Umoja wa Waandishi wa Habari mkoani Mbeya wakilaani mauaji kwa waandishi wa habari pamoja na vitisho wanavyotishiwa na vyombo vya usalama mara baada ya mwandishi wa Habari Daud Mwangosi kuuawa katika kijiji cha Nyololo Wilayani Mufindi-Iringa Septemba 2, 2012. (Picha imechukuliwa Mbeya Yetu Blog)

No comments: