NGUVU YA HABARI

Friday, December 26, 2014

Vionngozi wa kata ya Ihahi wajimilikisha ardhi ya umma zaidi ya ekari 100



Mbarali, Mbeya

Viongozi wa kata ya Ihahi wanadaiwa kujimilikisha zaidi ya ekari mia moja za mashamba ya umma katika eneo la bwawa la mhindi katika kijiji cha Ihahi wilayani Mbarali, mkoa Mbeya bila kuwashirikisha wananchi wa kata hiyo.

Baadhi ya wananchi wakizungumza na Mwandishi wetu wamesema viongozi wa kata ya Ihahi wilayani Mbarali wamejimilikisha ardhi yenye zaidi ya ekari mia moja katika bwawa la mhindi bila kuwahusisha.

Wananchi hao wamesema uchu wa madaraka, ubinafsi na kukosa uzalendo kwa viongozi walio wengi kumesababisha viongozi kutumia ardhi ya umma kwa maslahi yao binafsi.

Mwandishi wetu akaanza kwa kuitafuta serikali kupitia ofisi ya afisa mtendaji wa kata hiyo ili kujua ikiwa ni kweli ardhi hiyo imegawiwa kwa baadhi ya wananchi, viongozi wa kijiji na kata hiyo na akaanza kwa kubainisha kuwa madai ya wananchi hao yamefikishwa katika uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali.

Hata hivyo, afisa mtendaji wa kata ya Ihahi Costantino Tandika wakati akijibu tuhuma za uongozi wa kijiji na kata amesema kuna baadhi ya wananchi wamejimilikisha ardhi ya kijiji kinyume cha sheria na taratibu.
Naye aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji kabla ya uchaguzi Disemba 14, mwaka huu, Juma Mwahande amekanusha madai hayo huku akidai kuwa aliingia madarakani wakati ardhi hiyo eneo la Bwawa la mhindi ilikuwa imegawiwa kwa kufuata sheria na taratibu za ardhi.

Afisa mtendaji wa kijiji cha Ihahi Abraham Shangwa amesema yeye ni mgeni, hivyo bado hajapata taarifa zozote kuhusu mgogoro wa ardhi hiyo.

Wilaya ya mbarali ni moja ya wilaya mkoani mbeya ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha shughuli za kimaendeleo hususani migogoro ya ardhi kama ilivyotokea katika kata ya Ihahi wakazi wasiopungua hamsini kulalamikia ugawaji wa ardhi hiyo wilayani hapa.



Wednesday, December 24, 2014

Wananchi wa kata ya Ihahi wambeza mtendaji wao kusaidia kuleta maendeleo katika kata yao



Mbarali, Mbeya
Afisa mtendaji wa kata ya Ihahi katika halmashauri a wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Costantino Tandika amewataka wananchi wa kata hiyo kushirikiana na viongozi ili kuleta maendeleo ya kata hiyo.

Afisa mtendaji Tandika amesema hayo wakati akizungumza na redio Ushindi katika kijiji na kata ya Ihahi wilayani Mbarali katika mahojiano maalumu baada ya redio Ushindi kutembelea vijiji kadhaa vya kata hiyo.

Amesema ili jamii au taifa lo lote liendelea kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni lazima kuwepo na mshikamano na ushirikiano baina ya viongozi na wananchi katika shughuli za kimaendeleo.

Aidha amesema ushirikiano walioupata kutoka katika ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya mbarali umechangia kuinua maendeleo ya kijiji na kata yake ikiwemo ujenzi wa shule ya msingi na sekondari, zahanati pamoja na ofisi ya Kata hiyo.

Hata hivyo kauli ya mtendaji huyo wa kata imepingwa na wananchi wa Ihahi kuwa maendeleo bado ni duni hususani huduma ya maji, shule na shughuli mbalimbali za maendeleo ya kijiji na kata hiyo.
Aidha wananchi hao wamesema viongozi wa kata hiyo kutanguliza mbele masilahi yao kuchangia kurudisha nyuma maendeleo ya kata hiyo.

Baadhi ya tuhuma kama za tatizo la maji na kijiji cha Ihahi kutoendelea kwa kiwango kikubwa zikaelekezwa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji Juma Mwahande na afisa mtendaji wa kijiji hicho Abraham Shangwa aliyedai kuwa yeye ni mgeni kwani ameanza kazi hapo mwaka jana.

Kwa upande wake aliyekuwa mtendaji wa kijiji hicho kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa disemba 14 mwaka huu Juma Mwahande anmekanusha tuhuma zilizotolewa dhidi yake.

Wananchi ambao ni waajiri wakuu wa viongozi wanaowachagua wanategemea vitu gani watafanyiwe na viongozi wao?
Kata ya Ihahi iliyopo Chimala wilayani Mbarali ina jumla ya vijiji vitatu ambavyo ni Mwaluma, Ihahi na kijiji cha Kibaoni ikiwa na wakazi wasiopungua elfu sita (6000) ambao huduma ya maji wanategemea visima na mifereji inayopeleka maji katika mashamba ya wawekezaji wilayani humo.

     By  Josea Sinkala.