NGUVU YA HABARI

Friday, December 26, 2014

Vionngozi wa kata ya Ihahi wajimilikisha ardhi ya umma zaidi ya ekari 100



Mbarali, Mbeya

Viongozi wa kata ya Ihahi wanadaiwa kujimilikisha zaidi ya ekari mia moja za mashamba ya umma katika eneo la bwawa la mhindi katika kijiji cha Ihahi wilayani Mbarali, mkoa Mbeya bila kuwashirikisha wananchi wa kata hiyo.

Baadhi ya wananchi wakizungumza na Mwandishi wetu wamesema viongozi wa kata ya Ihahi wilayani Mbarali wamejimilikisha ardhi yenye zaidi ya ekari mia moja katika bwawa la mhindi bila kuwahusisha.

Wananchi hao wamesema uchu wa madaraka, ubinafsi na kukosa uzalendo kwa viongozi walio wengi kumesababisha viongozi kutumia ardhi ya umma kwa maslahi yao binafsi.

Mwandishi wetu akaanza kwa kuitafuta serikali kupitia ofisi ya afisa mtendaji wa kata hiyo ili kujua ikiwa ni kweli ardhi hiyo imegawiwa kwa baadhi ya wananchi, viongozi wa kijiji na kata hiyo na akaanza kwa kubainisha kuwa madai ya wananchi hao yamefikishwa katika uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali.

Hata hivyo, afisa mtendaji wa kata ya Ihahi Costantino Tandika wakati akijibu tuhuma za uongozi wa kijiji na kata amesema kuna baadhi ya wananchi wamejimilikisha ardhi ya kijiji kinyume cha sheria na taratibu.
Naye aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji kabla ya uchaguzi Disemba 14, mwaka huu, Juma Mwahande amekanusha madai hayo huku akidai kuwa aliingia madarakani wakati ardhi hiyo eneo la Bwawa la mhindi ilikuwa imegawiwa kwa kufuata sheria na taratibu za ardhi.

Afisa mtendaji wa kijiji cha Ihahi Abraham Shangwa amesema yeye ni mgeni, hivyo bado hajapata taarifa zozote kuhusu mgogoro wa ardhi hiyo.

Wilaya ya mbarali ni moja ya wilaya mkoani mbeya ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha shughuli za kimaendeleo hususani migogoro ya ardhi kama ilivyotokea katika kata ya Ihahi wakazi wasiopungua hamsini kulalamikia ugawaji wa ardhi hiyo wilayani hapa.



No comments: