NGUVU YA HABARI

Monday, September 29, 2014

WANANCHI WA SONGWE WAANDAMANA KWA MKUU WA WILAYA YA MBEYA KUSHINIKIZA WALIPWE FIDIA ZAO

Wananchi wa kitongaji cha Kaloleni kijiji cha Songwe wilaya ya Mbeya vijijini wameandamana hadi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Mbeya wakida kulipwa fidia ya maeneo yao yaliochukuliwa na serikali kwa ajili ya kupisha ujenzi wa nyumba za Taifa NHC tangu mwaka 2013.
Wakizungumza na vyombo vya habari mapema septemba 29 mwaka huu,wananchi hao walisema kuwa waliahidiwa na serikali kulipwa fidia zao ndani ya miezi mitatu mara tu baada ya maeneo yao kufanyiwa tathmini na serikali kinyume chake mpaka sasa ni mwaka mmoja umepita bila kulipwa ya malipo hayo.
Aidha wakitoa malalamiko hayo kwa mkuu wa wilaya ya Mbeya Dk. Norman Sigalla walisema tangu kufanyiwa kwa tathmini ya maeneo hayo wamezuiliwa kufanya shughuli yoyote katika maeneo hayo ambapo wamedai hata vyoo vimeharibika lakini wanashindwa kujenga vingine kutokana na zuio hilo hali inayopelekelea kuhatarisha usalama wa afya zao.
Walimweleza mkuu wa wilaya kuwa wananchi wengi hawakuwa tayari kukubali kutoa eneo hilo kwa shirika la nyumba bila shinikizo lake na kuongeza kuwa yeye ndiye aliyewathibitishia kulipwa fidia zao ndani ya muda wa miezi mitatu tangu mwezi Agosti 19 mwaka jana.
Naye, diwani wa kata ya Bonde la Songwe Amon Jacob Mwakapala alisema wananchi wamekosa imani naye kutokana na serikali kushindwa kutekeleza ahadi ya kuwalipa fidia ndani ya miezi mitatu.
Akijibu tuhuma hizo mkuu wa wilaya ya Mbeya Norman Sigalla alikiri kucheleweshwa kwa wananchi hao juu ya stahiki zao huku akidai kuwa aliwasiliana na shirika la nyumba la Taifa NHC Makao makuu jijini Dar es Salaam  na kudaiwa kuwa madai ya wananchi hao yamefikia kwenye hatua ya uhakiki na kuwaahidi kuwa atahakikisha wananchi hao wanalipwa fidia zao mwezi ujao.
Aidha Sigalla aliwataka wananchi hao kuwa na subira wakati madai yao yakiendelea kushughulikia na serikali.

Hata hivyo wananchi hao walikubaliana na kauli ya mkuu wa wilaya kusubiri huku wakitoa masharti kuwa endapo hatashughulikia swala hilo kwa muda wiki moja wataendelea na shughuli zao kama kawaida kwenye maeneo hayo.

No comments: