NGUVU YA HABARI

Friday, February 27, 2015

Wachungaji waonywa kupokea zawadi kwa Wanasiasa bila maelezo ya Kina



Na Petro Kalago, MBEYA      

Serikali imewataka viongozi wa dini kuwa makini na wanasiasa ambao hukimbilia kutoa misaada makanisani wakati uchaguzi unapokaribia kwa ajili ya kujitafuatia umaarufu.

Akihutubia katika kongamano lililowakutanisha viongozi wa dini ya kikristo na kiislam februari 26 mwaka huu Mkurugenzi wa taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya Felix Wandwe, amesema viongozi wa dini wawe makini kwa kipindi hiki cha uchaguzi kwani baadhi ya watu hujipendekeza kwa kutoa misaada bila sababu.

Aidha, amesema kuwa Mwaka huu watanzania wana mambo makuu matatu wanayotarajia kuyafanya ambayo ni Uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura, kuipigia kura ya maoni katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi oktoba mwaka huu.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Mbeya Samora Saranga akihutubia katika kongamano hilo kwa niaba ya kamanda wa jeshi polisi mkoa Ahmed Msangi amesema kuwa matukio ya uharifu katika Mkoa wa Mbeya yameendelea kuongezeka kutoka Mwaka 2013-2014  kwa kiasi kikubwa na kusema kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kukemea maovu yanayojitokeza katika jamii.

Sambamba na hayo wametoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura pia kushiriki kikamilifu katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba mwaka huu bila kathiri Amani ya Taifa.

Wananchi wataka Ushirikiano Udumishwe baina yao na Viongozi wa serikali za Mitaa



Na Atu Mbotwa, MBEYA  

Baadhi ya wakazi wa jiji la Mbeya wamewalalamikia viongozi wa Serikali za mitaa kwa kutoa maamuzi kuhusu mipango ya maendeleo bila kuwashirikisha wananchi.

Wamesema hayo Februari 26, mwaka huu kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na Nguvu ya Habari ambapo wamesema kuwa migogoro mingi hujitokeza kutokana na viongozi kufanya maamuzi yanayogusa mustakabali wa wananchi bila kuzingatia maoni ya wananchi husika.

Kwa upande wao wenyeviti wa mitaa ya Sokoni na Mponja wamekiri kuwepo kwa tatizo hilo kwa baadhi ya viongozi, jambo ambalo wameeleza kuwa ni kinyume cha Sheria na maadili ya uongozi.

Wamesema kuwa, Sheria inawataka viongozi wa mitaa kuandaa angalau mikutano sita kwa mwaka kwa ajili ya kujadili na wananchi kuhusu mipango ya mtaa husika.

Kwa Mujibu wa Katiba, Wajibu na Haki ya kila Mwananchi katika Kijiji ni Kuhudhuria mikutano yote katika kitongoji, kijiji na mtaa na kuhakikisha kuwa mikutano inafanyika kila baada ya muda uliopangwa, Kulinda mali, rasilimali za umma na kupambana na kila aina ya uovu ikiwemo ubadhirifu, wizi, rushwa na mengineyo.

Pia, Kumwondoa kiongozi au viongozi wasiowajibika kwa kumpigia kura ya hapana, Kujenga na kuimarisha mshikamano uliopo katika jamii yake, Kushiriki kupanga, kusimamia na kuthathimini na kuhoji matokeo ya miradi yote katika kitongoji, kijiji na mtaa, Kushiriki katika kupiga na kupigiwa kura kugombea nafasi za uongozi na Kuheshimu kiongozi au viongozi wake.

Hivyo Kwa mujibu wa Katiba ni kosa kwa Kiongozi wa Serikali ya Mtaa, Kijiji na Kitongoji kufanya shughuli za mtaa bila kuwashirikisha wananchi wa mtaa husika.



Wanafunzi sita Wabakwa kwa Nyakati Tofauti mkoani Mbeya



Na Josea Sinkala, MBEYA

Afisa mtendaji wa mtaa wa Hayanga kata ya Ilomba jijini Mbeya Maria Mwaiswelo ameitaka jamii kuwa na mwamko mpya wa kutoa taarifa za kuwepo kwa matukio yanayotokea katika maeneo yao kwenye vyombo vinavyohusika kwa hatua zaidi za kisheria.

Mwaiswelo ametoa rai hiyo February 27 mwaka huu alipotembelewa na Nguvu Ya Habari ofisini kwake kufuatia kuwepo kwa tukio la mtu mmoja kutuhumiwa kuwabaka watoto kadhaa katika mtaa huo bila kitendo hicho kufikishwa katika ngazi zinazohusika.

Maria amesema ofisi yake haina taarifa yoyote ya kuwepo kwa mtu aliyewabaka watoto wanaokadiliwa kuwa sita katika mtaa huo hivyo amesema hawezi kuzungumzia zaidi tukio hilo huku akiitaka jamii kutoa taarifa juu ya kuwepo kwa vitendo kama hivyo badala ya kutaka kumaliza masuala hayo kindugu.

Mmoja wa watoto hao mwenye umri wa miaka saba (7) na mwanafunzi wa shule ya msingi Ikulu wanaodaiwa kubakwa na kuchezewa na mtuhumiwa anayeelezwa kutenda vitendo hivyo kwa nyakati tofauti ameiambia Nguvu ya Habari kuwa alikuwa akiitwa na mtuhumiwa na kuanza kumfanyia vitendo hivyo akimlaghai kwa kumpatia fedha kiasi cha shilingi hamsini.

Naye mama mzazi wa mtoto huyo (Jina limehifadhiwa) akizungumzia tukio hilo Amesema baada ya kupata taarifa juu ya mwanae kutendewa kitendo hicho alimjulisha mume wake kwa kuwa hakuwepo nyumbani ndipo wakaenda kutoa taarifa kwa balozi wa mtaa huo na kwamba hatua zilikuwa bado hazijaanza kuchukuliwa.

Amedai kusikitishwa na kitendo hicho ambapo ameiomba serikali na vyombo vinavyohusika kumsaidia kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria ikiwemo kukamatwa kwa mtuhumiwa na kwamba wanafanya taratibu kwa ajili ya kumpeleka mtoto wao hospitali kwa uchunguzi zaidi wa kiafya.

Mwenyekiti wa mtaa huo Godliving Paul Koka amesema taarifa rasmi za tukio hilo hajizamfikia na kuahidi kushirikiana na viongozi wengine pamoja na wananchi ili kuhakikisha mtuhumiwa anachukuliwa hatua za kisheria.

Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamesema vitendo kama hivyo havitakiwi kufumbiwa macho ambapo mtuhumiwa huyo aliyetajwa kwa jina la Lukas Mwangono amekuwa akifanya vitendo hivyo kwa muda mrefu ambavyo vimekuwa kero kwa ndugu na majirani wa mtaa huo.

Aidha wamesema mtuhumiwa amekuwa na kawaida ya kuwachezea watoto wa ndugu zake hivyo kutotafuta hatua zaidi za ufumbuzi bali wamekuwa wakiyamaliza masuala hayo kifamilia tofauti na awamu hii ambapo baada ya kikao cha baadhi ya wananchi kilichofanyika February 26 mwaka huu mtuhumiwa alikimbia na haijulikani aliko.

Hata hivyo mtuhumiwa huyo Lukas Mwangomo alipopigiwa simu kujibu tuhuma hizo amegoma kujibu tuhuma zinazo mkabili.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya Kupitia Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Samora Saranga amwesema Jeshi la Polisi haliwezi kuchukua hatua zozote kwakuwa tukio hilo halijaripotiwa Polisi, hivyo kuwataka wazazi wa watoto waliokumbwa na mkasa huo kutoa taarifa katika vyombo vinavyohusika.


Thursday, February 26, 2015

Wananchi Mkoani Mbeya Wapigwa Marufuku Kujenga Nyumba Eneo la Kilimo



Na Elizabeth Nyivambe, MBEYA                 

Baadhi ya viongozi wa shirika la mradi wa umwagiliaji bonde la Uyole, kata ya Iganju, jijini Mbeya wamewataka wananchi kutojenga nyumba katika maeneo ya bonde hilo kwa madai kuwa maeneo hayo ni kwaajili ya kilimo tu.

Viongozi hao wakizungumza na Nguvu ya Habari, Februari 26, mwaka huu kwa nyakati tofauti, wamesema kuwa maeneo hayo yametengwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na siyo ujenzi wa makazi ya watu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa shirika hilo John Soda amesema kuwa kuna watu wachache ambao wameingia kujenga katika maeneo ya umwagiliaji hivyo ametoa tahadhari kwa wale wote ambao wamejenga kwenye maeneo hayo kuwa muda wowote majengo hayo yatabomolewa.

Nguvu ya Habari imefanikiwa kuongea na baadhi ya wananchi waliojenga katika eneo la umwagiliaji ambao wamesema kuwa wakati wananunua maeneo hayo hawakujua kuwa ni maeneo ya umwagiliaji.

Pia wamesema kuwa walimwandikia barua Diwani wa kata hiyo kuomba maeneo yaliyojengwa yabaki kuwa maeneo ya makazi na sio ya umwagiliaji lakini mpaka sasa hawajajibiwa.

Naye Diwani wa kata ya Iganju, Boniface James Jumbo amesema kuwa alipokea barua kutoka kwa mkurugenzi wa jiji ambayo imewaruhusu wananchi ambao wamejenga kuendelea kuishi na kwa wale wenye maeneo ya wazi wasiendeleleze ujenzi wowote.

Hata hivyo viongozi hao wametoa wito kwa wananchi kuacha kujenga kwenye maeneo ya umwagiliaji pia wamewataka wale wote wanaonunua maeneo katika hifadhi hiyo ni vema wawaone viongozi wa shirika la umwagiliaji ili kujua taratibu za maeneo hayo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu 25



  Na Faraja Muwanje, MBEYA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu 25 Raia wa Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa Mbeya Ahmed Msangi amesema raia hao wamekamatwa wakiwa wamefichwa kwenye nyumba ya mwananchi ambaye ni mkazi wa uyole.

Wahamiaji hao wanadaiwa kuingia Nchi bila vibali, ikiwa ni siku tatu zimepita tangu watu wengine 75 walipokamatwa mjini Mbeya wakijaribu kuvuka mpaka kuelekea  Nchi za Kusini.

Idadi ya watu wanaoingia nchini wakielekea Nchi za kusini imezidi kuongezeka hali inayotishia usalama na amani kwa maeneo yaliyokuwa pembezoni ikiwemo wilaya ya Ileje na Momba Mkoani Mbeya.

Kamanda  Ahmedi Msangi amesema unahitajika uzalendo katika kudhibiti na kukomesha misafara ya watu wanaoingia Nchini bila vibali.