Na Elizabeth
Nyivambe, MBEYA
Baadhi ya viongozi wa shirika la mradi wa umwagiliaji
bonde la Uyole, kata ya Iganju, jijini Mbeya wamewataka wananchi kutojenga nyumba
katika maeneo ya bonde hilo kwa madai kuwa maeneo hayo ni kwaajili ya kilimo
tu.
Viongozi hao wakizungumza na Nguvu ya Habari, Februari
26, mwaka huu kwa nyakati tofauti, wamesema kuwa maeneo hayo yametengwa kwa
ajili ya kilimo cha umwagiliaji na siyo ujenzi wa makazi ya watu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa shirika hilo John
Soda amesema kuwa kuna watu wachache ambao wameingia kujenga katika maeneo ya
umwagiliaji hivyo ametoa tahadhari kwa wale wote ambao wamejenga kwenye maeneo
hayo kuwa muda wowote majengo hayo yatabomolewa.
Nguvu ya Habari imefanikiwa kuongea na baadhi ya
wananchi waliojenga katika eneo la umwagiliaji ambao wamesema kuwa wakati
wananunua maeneo hayo hawakujua kuwa ni maeneo ya umwagiliaji.
Pia wamesema kuwa walimwandikia barua Diwani wa
kata hiyo kuomba maeneo yaliyojengwa yabaki kuwa maeneo ya makazi na sio ya
umwagiliaji lakini mpaka sasa hawajajibiwa.
Naye Diwani wa kata ya Iganju, Boniface James
Jumbo amesema kuwa alipokea barua kutoka kwa mkurugenzi wa jiji ambayo
imewaruhusu wananchi ambao wamejenga kuendelea kuishi na kwa wale wenye maeneo
ya wazi wasiendeleleze ujenzi wowote.
Hata hivyo viongozi hao wametoa wito kwa wananchi
kuacha kujenga kwenye maeneo ya umwagiliaji pia wamewataka wale wote wanaonunua
maeneo katika hifadhi hiyo ni vema wawaone viongozi wa shirika la umwagiliaji
ili kujua taratibu za maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment