NGUVU YA HABARI

Friday, December 26, 2014

Vionngozi wa kata ya Ihahi wajimilikisha ardhi ya umma zaidi ya ekari 100



Mbarali, Mbeya

Viongozi wa kata ya Ihahi wanadaiwa kujimilikisha zaidi ya ekari mia moja za mashamba ya umma katika eneo la bwawa la mhindi katika kijiji cha Ihahi wilayani Mbarali, mkoa Mbeya bila kuwashirikisha wananchi wa kata hiyo.

Baadhi ya wananchi wakizungumza na Mwandishi wetu wamesema viongozi wa kata ya Ihahi wilayani Mbarali wamejimilikisha ardhi yenye zaidi ya ekari mia moja katika bwawa la mhindi bila kuwahusisha.

Wananchi hao wamesema uchu wa madaraka, ubinafsi na kukosa uzalendo kwa viongozi walio wengi kumesababisha viongozi kutumia ardhi ya umma kwa maslahi yao binafsi.

Mwandishi wetu akaanza kwa kuitafuta serikali kupitia ofisi ya afisa mtendaji wa kata hiyo ili kujua ikiwa ni kweli ardhi hiyo imegawiwa kwa baadhi ya wananchi, viongozi wa kijiji na kata hiyo na akaanza kwa kubainisha kuwa madai ya wananchi hao yamefikishwa katika uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali.

Hata hivyo, afisa mtendaji wa kata ya Ihahi Costantino Tandika wakati akijibu tuhuma za uongozi wa kijiji na kata amesema kuna baadhi ya wananchi wamejimilikisha ardhi ya kijiji kinyume cha sheria na taratibu.
Naye aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji kabla ya uchaguzi Disemba 14, mwaka huu, Juma Mwahande amekanusha madai hayo huku akidai kuwa aliingia madarakani wakati ardhi hiyo eneo la Bwawa la mhindi ilikuwa imegawiwa kwa kufuata sheria na taratibu za ardhi.

Afisa mtendaji wa kijiji cha Ihahi Abraham Shangwa amesema yeye ni mgeni, hivyo bado hajapata taarifa zozote kuhusu mgogoro wa ardhi hiyo.

Wilaya ya mbarali ni moja ya wilaya mkoani mbeya ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha shughuli za kimaendeleo hususani migogoro ya ardhi kama ilivyotokea katika kata ya Ihahi wakazi wasiopungua hamsini kulalamikia ugawaji wa ardhi hiyo wilayani hapa.



Wednesday, December 24, 2014

Wananchi wa kata ya Ihahi wambeza mtendaji wao kusaidia kuleta maendeleo katika kata yao



Mbarali, Mbeya
Afisa mtendaji wa kata ya Ihahi katika halmashauri a wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Costantino Tandika amewataka wananchi wa kata hiyo kushirikiana na viongozi ili kuleta maendeleo ya kata hiyo.

Afisa mtendaji Tandika amesema hayo wakati akizungumza na redio Ushindi katika kijiji na kata ya Ihahi wilayani Mbarali katika mahojiano maalumu baada ya redio Ushindi kutembelea vijiji kadhaa vya kata hiyo.

Amesema ili jamii au taifa lo lote liendelea kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni lazima kuwepo na mshikamano na ushirikiano baina ya viongozi na wananchi katika shughuli za kimaendeleo.

Aidha amesema ushirikiano walioupata kutoka katika ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya mbarali umechangia kuinua maendeleo ya kijiji na kata yake ikiwemo ujenzi wa shule ya msingi na sekondari, zahanati pamoja na ofisi ya Kata hiyo.

Hata hivyo kauli ya mtendaji huyo wa kata imepingwa na wananchi wa Ihahi kuwa maendeleo bado ni duni hususani huduma ya maji, shule na shughuli mbalimbali za maendeleo ya kijiji na kata hiyo.
Aidha wananchi hao wamesema viongozi wa kata hiyo kutanguliza mbele masilahi yao kuchangia kurudisha nyuma maendeleo ya kata hiyo.

Baadhi ya tuhuma kama za tatizo la maji na kijiji cha Ihahi kutoendelea kwa kiwango kikubwa zikaelekezwa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji Juma Mwahande na afisa mtendaji wa kijiji hicho Abraham Shangwa aliyedai kuwa yeye ni mgeni kwani ameanza kazi hapo mwaka jana.

Kwa upande wake aliyekuwa mtendaji wa kijiji hicho kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa disemba 14 mwaka huu Juma Mwahande anmekanusha tuhuma zilizotolewa dhidi yake.

Wananchi ambao ni waajiri wakuu wa viongozi wanaowachagua wanategemea vitu gani watafanyiwe na viongozi wao?
Kata ya Ihahi iliyopo Chimala wilayani Mbarali ina jumla ya vijiji vitatu ambavyo ni Mwaluma, Ihahi na kijiji cha Kibaoni ikiwa na wakazi wasiopungua elfu sita (6000) ambao huduma ya maji wanategemea visima na mifereji inayopeleka maji katika mashamba ya wawekezaji wilayani humo.

     By  Josea Sinkala.

Monday, September 29, 2014

WANANCHI WA SONGWE WAANDAMANA KWA MKUU WA WILAYA YA MBEYA KUSHINIKIZA WALIPWE FIDIA ZAO

Wananchi wa kitongaji cha Kaloleni kijiji cha Songwe wilaya ya Mbeya vijijini wameandamana hadi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Mbeya wakida kulipwa fidia ya maeneo yao yaliochukuliwa na serikali kwa ajili ya kupisha ujenzi wa nyumba za Taifa NHC tangu mwaka 2013.
Wakizungumza na vyombo vya habari mapema septemba 29 mwaka huu,wananchi hao walisema kuwa waliahidiwa na serikali kulipwa fidia zao ndani ya miezi mitatu mara tu baada ya maeneo yao kufanyiwa tathmini na serikali kinyume chake mpaka sasa ni mwaka mmoja umepita bila kulipwa ya malipo hayo.
Aidha wakitoa malalamiko hayo kwa mkuu wa wilaya ya Mbeya Dk. Norman Sigalla walisema tangu kufanyiwa kwa tathmini ya maeneo hayo wamezuiliwa kufanya shughuli yoyote katika maeneo hayo ambapo wamedai hata vyoo vimeharibika lakini wanashindwa kujenga vingine kutokana na zuio hilo hali inayopelekelea kuhatarisha usalama wa afya zao.
Walimweleza mkuu wa wilaya kuwa wananchi wengi hawakuwa tayari kukubali kutoa eneo hilo kwa shirika la nyumba bila shinikizo lake na kuongeza kuwa yeye ndiye aliyewathibitishia kulipwa fidia zao ndani ya muda wa miezi mitatu tangu mwezi Agosti 19 mwaka jana.
Naye, diwani wa kata ya Bonde la Songwe Amon Jacob Mwakapala alisema wananchi wamekosa imani naye kutokana na serikali kushindwa kutekeleza ahadi ya kuwalipa fidia ndani ya miezi mitatu.
Akijibu tuhuma hizo mkuu wa wilaya ya Mbeya Norman Sigalla alikiri kucheleweshwa kwa wananchi hao juu ya stahiki zao huku akidai kuwa aliwasiliana na shirika la nyumba la Taifa NHC Makao makuu jijini Dar es Salaam  na kudaiwa kuwa madai ya wananchi hao yamefikia kwenye hatua ya uhakiki na kuwaahidi kuwa atahakikisha wananchi hao wanalipwa fidia zao mwezi ujao.
Aidha Sigalla aliwataka wananchi hao kuwa na subira wakati madai yao yakiendelea kushughulikia na serikali.

Hata hivyo wananchi hao walikubaliana na kauli ya mkuu wa wilaya kusubiri huku wakitoa masharti kuwa endapo hatashughulikia swala hilo kwa muda wiki moja wataendelea na shughuli zao kama kawaida kwenye maeneo hayo.

Sunday, August 31, 2014

WATANZANIA WAASWA KUACHA TABIA YA KUBAGUANA KIIMANI


Watanzania wametakiwa wajibidishe kumcha mungu ili wapate malipo mema baadaye na kuacha tabia kubaguana, kulumbana kwa sababu ya tofauti za imani yao ya dini.

Nasaha hizo amezitoa pandre Emillius Haule wa kanisa la Anglikana la Mwenge wakati wa ibada ya mazishi ya Bw. Dunstan Cuthbert Shaban aliyekuwa msajili wa kwanza wa bodi ya taifa ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu - NBAA, aliyefariki jumanne wiki hii.

Wakizungumza katika maziko hayo mwenyekiti wa zamani wa bodi ya NBAA Dr Reginald Mengi, na mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali Bw. Ludovick Utouh wamesema wakati wa uhai wake  marehemu Dunstan Shaban alikuwa mtu mwema, muadilifu na mchapakazi hodari aliyejitoa kulitumikia taifa lake.

Aidha katika salamu zao za rambirambi mkurugenzi wa NBAA Bw. Pius Maneno, na mwenyekiti wa bodi ya kituo cha kutoa elimu kiitwacho the Universal Education Centre Bw. Boko William Boko wamesema marehemu atakumbukwa kwa uzalendo wake na mambo mengine mazuri aliyoyafanya  wakati wa uhai wake

Wednesday, August 20, 2014

AZAM FC YAANGUKIA PUA NUSU FAINALI KAGAME

MABINGWA wa Tanzania, Azam fc waaga rasmi mashindano ya kombe la Afrika Mashariki na kati maarufu Kombe la Kagame kwa baada ya kunyukwa  penati 4-3 dhidi ya El Merreik ya Sudan  katika mchezo wa robo fainali.
Mshindi wa mchezo huo uliopigwa katika dimba la Nyamirambo mjini Kigali, Rwanda, hadi dakika 90 zinakamilika Azam FC 0 na El Merreikh 0.
Mikwaju ya matuta ikaleta kilio kwa Azam baada ya dakika 90 kumalizika kwa timu hizo kutotikisa nyavu za ngoli la mwenzake (0-0).
Azam FC walioneka kutokuwa na bahati ya kuchekelea nyavu za El Merreik baada ya washambuliaji Kipre Herman Tchetche, John Bocco na Leonel Saint-Prexu kutotumia vema nafasi walizopata.
Katika hatua ya matuta Azam FM wanalambalamba walipata penati 3 ambazo zilifungwa na Aggrey Morris, Didier Kavumbagu na Erasto Edward Nyoni, huku wachezaji wake Shomari Salum Kapombe na Leonel Saint- Prexu ndiyo waliopeleka kilio Azam FC baada ya kukosa penalti zao.
Katika mchezo mwingine wa KCCA na ATLabara, Timu ya KCCA imeichalaza timu ya Atlabara magoli 3 kwa 1, na kufanikiwa kutinga nusu fainali.
Kwa matokeo hayo ya leo, Nusu fainali itazikutanisha timu mbili za Rwanda, Polisi na APR na timu ya El Merreckh itachuana na timu ya KCCA.

OFISI ZA SHIRIKISHO KA SOKA LA nIGERIA ZA TEKETEA KWA MOTO

Iliwachukua zaidi ya saa mbili kwa zima moto wakisaidiana na umma kuuzima moto huo mkubwa .
Ofisa wa zima moto Eyo Ime akiongea na BBC alisema kuwa wanashuku chanzo cha moto huo ulitokana na hitilafu ya umeme.
Katibu mkuu wa NFF bwana Musa Amadu alisema kuwa moto huo ulianzia katika ofisi ya mhasibu wa shirikisho hilo.
Amadu akiongea na BBC alisema anashukuru mungu kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha yake kutokana na moto huo kwa hivyo hakuna faida ya kumlaumu mtu yeyote.
Mkasa huo wa moto ni pigo kwa shirikisho hilo ambalo tayari linakabiliwa na mvutano wa uongozi ambao umepelekea kung'olewa madarakani kwa mwenyekiti Aminu Maigari mara mbili akirejeshwa.
Ofisi iliyoko sasa haijatia sahihi makubaliano yeyote wala mkataba na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Stephen Keshi ambaye aliiongoza timu hiyo kuenda kwenye kombe la dunia huko Brazil.

Keshi mwenyewe aliiambia BBC kuwa anatarajia kukamilisha mazungumzo kati ya saa 24 hadi 48 zijazo.

Saturday, August 2, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI,

DAR ES SALAAM, ALHAMISI, 31 JULAI 2014 SAA 5.00 ASUBUHI.


Ndugu waandishi wa habari,

Kama mnavyofahamu Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba (BMK) wanaotetea kuheshimiwa kwa maoni ya Wananchi katika mchakato wa kuandika Katiba maarufu kwa jina la UKAWA- Umoja wa Katiba ya Wananchi walitoka nje ya Bunge hilo tarehe 16 April 2014.

Sababu ya msingi iliyotutoa kwenye BMK ni mkakati uliokuwa ukitekelezwa na Wajumbe wa BMK wa CCM kupuuza maoni ya wananchi yaliyokusanywa na kuratibiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikiongozwa na Mwenyekiti Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu mwenyekiti Jaji Agostino Ramadhani. Rasimu ya Katiba inapendekeza Muundo wa Muungano wa Shirikisho yenye Serikali Tatu. Kama waraka wa CCM unavyoeleza “Muundo wa Muungano ndiyo moyo wa Rasimu na ndiyo unaoamua ibara nyingine zikae vipi.” CCM wameukataa Muundo wa Muungano uliopendekezwa na Tume, na badala yake wanataka Muundo wa Serikali mbili ambao haujafanyiwa utafiti, haujapendekezwa na wananchi walio wengi, uliojaa na matattizo lukuki yasiyotatulika tangu enzi za uhuru na ambao haujapendekezwa na tume ya mabadiliko ya katiba. Kwa sababu aina ya muundo wa muungano ndiyo moyo wa rasimu ya katiba(kwa tafsiri ya CCM), ukiunyonga Moyo wa Rasimu hautakuwa na Rasimu ya Katiba inayotokana na maoni ya wananchi. UKAWA tunatetea maoni ya Wananchi yaheshimiwe na tumetoa wito kila mara kuwa hii ndiyo njia bora ya kutufanya turidhiane.

Ikumbukwe kuwa bunge la katiba halikuanzisha mchakato wa katiba, linakamilisha moja ya hatua muhimu za kupata katiba, tayari hatua mbili muhimu zimeshafanyika, maoni ya wananchi yametolewa na tume imetumia maoni hayo pamoja na rejea zingine na historia mbalimbali na imetuletea rasimu ya katiba inayotokana na mambo hayo. Bunge Maalum la Katiba halina uwezo na kibali cha kuvunja misingi mikuu ya maoni ya wananchi na kazi ya tume, kuvunja misingi mikuu “moyo wa rasimu” ni sawa na kuanzisha mchakato mwingine wa katiba na ni sawa na kuwa juu ya maoni na matakwa ya wananchi – UKAWA tumekataa kuwa sehemu ya uchakachuaji huu wa hali ya juu.

Ndugu waandishi wa habari,

Tunapenda ifahamike kuwa, UKAWA pia tulikwazwa na lugha za ubaguzi, uchochezi, matusi na kejeli zilizokuwa zikiporomoshwa na baadhi ya Wajumbe wa CCM ndani na nje ya BMK. Michango mingi ya Wajumbe wa CCM wa Bunge Maalum ilikuwa ya kumkejeli na kumdhalilisha Jaji Joseph Sinde Warioba na kauli za kibaguzi dhidi ya Waarabu, Wapemba na Wahindi.

Lugha za kibaguzi na kichochezi pia zilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi alipokuwa anamwakilisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika ibada ya kumsimika Askofu wa Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma. Mhe. Lukuvi aliwataka wananchi waliohudhuria ibada hiyo kupinga serikali tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa Serikali ya Muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi. Katika hotuba yake katika kanisa la Methodist Mhe. Lukuvi aliendelea kuwachochea waumini aliposema kuwa “Serikali tatu zikipita ni wazi kuwa hata makanisa yatafungwa kwani nchi haiwezi kuwa na amani tena.”

Lukuvi alisema Wazanzibari wanaotaka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali wanataka Serikali ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa ni nchi ya Kiislamu. Serikali haikuchukua hatua yeyote kukanusha na kumuwajibisha Mhe. Lukuvi.

Hivi karibuni kumekuwa na miito mbalimbali ambayo imetolewa kututaka sisi tulioko katika Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA), kurejea bungeni. Katika Baraza la IDD ambako Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikuwa mgeni rasmi wito wa UKAWA kurudi bungeni ulisisitizwa.

Watu wengi wametoa kauli na hasa baadhi ya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya kidini nchini, kututaka turejee bungeni ili kuendelea na mchakato wa kuandika katiba mpya. Tunasema, tumewasikia na tunaheshimu kauli zao.

Tunatambua kuwa viongozi wa kidini ni watu wenye heshima na nafasi ya pekee katika jamii yetu. Ni watu waliopewa wajibu wa kutuongoza tukiwa hapa duniani na hata tukiondoka duniani. Kwa hiyo, napenda kuwahakikishieni kabisa kuwa UKAWA inaheshimu sana miito na ushauri wao.

Ndugu waandishi wa habari,

Pamoja na heshima hiyo, tunapenda pia waelewe haya yafuatayo:

Kwanza, UKAWA uliondoka bungeni, pamoja na mengine, kupinga njama za kuhujumu mchakato wa Katiba Mpya. Tulipinga kudharauliwa maoni ya wananchi kama yalivyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba.

Tumepinga Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupuuza maoni ya wananchi na kutaka kuingiza maoni yake, kinyume cha kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Pili, tuliondoka bungeni kupinga lugha ya ubaguzi, uchochezi, matusi na kejeli. Baadhi ya kauli hizi tulizikabili ndani ya bunge na kuonya wenzetu kuacha lugha hizo na badala yake watumie jukwaa hilo kusaidia upatikanaji wa katiba mpya. Hatukusikilizwa.

Ninyi ni mashahidi jinsi wajumbe wa CCM walivyoporomosha matusi makubwa na tuhuma nzito dhidi ya Tume ya Jaji Warioba. Baadhi ya wajumbe waliwaita wajumbe wa tume hii Eti, “wasaliti wa Baba wa Taifa; wazee wanaosubiri kufa; na watu wasiokuwa na uzalendo bali wana ajenda binafsi.”

Tatu, tuliondoka bungeni baada ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Mhe. Samuel Sitta kushindwa kuwadhibiti wajumbe wanaotumia lugha ya ubaguzi, uchochezi, matusi na kejeli na kuendesha vikao vya bunge hilo kwa upendeleo. Mwenyekiti ameliendesha Bunge hilo kibabe. Ameshiriki kubadili ratiba na mtiririko wa matukio bungeni. Mwenyekiti wa Bunge la Katiba alivunja kanuni kwa kumtanguliza Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha Rasimu kabla Bunge kusikiliza hotuba ya ufunguzi ya Mgeni Rasmi. Amebadili Kanuni za Bunge la Katiba na sasa ametishia kufanya hivyo tena.

Nne, tuliondoka bungeni baada ya kuona waziri mmoja mwandamizi wa serikali ya Rais Kikwete, William Lukuvi, akiingia kanisani na kufanya uchochezi. Alidai Zanzibar inataka serikali tatu ili iwe huru kuanzisha Serikali ya Kiislamu na kuwarejesha Waraabu visiwani humo. Waziri huyu alikuwa amekwenda Kanisani kumwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Hadi tunaondoka na mpaka sasa, hakuna mamlaka yoyote iliyo juu ya Lukuvi ambayo imechukua hatua angalau hata ya kuomba radhi. Waziri Mkuu alikuwa na fursa adhimu kama mgeni rasmi katika Baraza la Idd kuomba radhi lakini hakufanya hivyo.

Tunawashukuru sana viongozi wa dini waliotoa matamko kulitaka Bunge Maalum la Katiba liheshimu maoni ya wananchi.

Ndugu waandishi wa habari,

Pamoja na kuwaheshimu viongozi wote wa dini, tumesikitishwa na matamshi ya baadhi yao kama yale yaliyotolewa katika Baraza la Idd kututaka UKAWA turejee bungeni, huku wakinyamazia matendo yaliyofanyika. Waziri Mkuu aliyekuwa mgeni rasmi katika Baraza la Idd ndiye aliyewakilishwa na Waziri Lukuvi alipotoa alipotoa kauli za kibaguzi na kichochezi katika kanisa la Methodist mjini Dodoma.

Leo ni zaidi ya miezi miwili tangu Bunge hili liahirishwe. Hatujamsikia kiongozi yoyote wa kidini (wale) wanaotutaka turudi bungeni, wakikemea au kutoa wito kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum kutumia haki, hekima na usawa, katika kuendesha mijadala bungeni.

Hatujasikia viongozi wa dini wanaotaka UKAWA warudi Bungeni wakitoa wito kwa wabunge wa chama tawala kurejea kwenye ajenda kuu na kuacha kashfa dhidi ya Tume. Kimya chao katika suala hili, kimechangia kukiongezea chama tawala kibri na dharau dhidi ya wananchi.

Vilevile, hatujawasikia viongozi wa madhehebu ya kidini wakimkemea Lukuvi wala Waziri Mkuu Pinda kuhusu kilichotokea kanisani Dodoma.

Badala yake, tumeendelea kuona viongozi wa dini wakikutana na viongozi wa serikali na chama tawala, bila jitihada za viongozi hao kukutana na UKAWA. Miito ya viongozi hawa inaelekezwa upande mmoja ikifumbia macho upande wa pili.

Sisi tunaamini viongozi wetu wa kiroho wanao uwezo wa kuangalia pande zote mbili na kutoa miito yenye ukweli, usawa na haki. Tunawasishi kabla ya kututaka kurejea bungeni, wangetumia busara hiyohiyo kutusikiliza na sisi kama ambavyo wanawafuata viongozi wa CCM, ofisi ndogo ya Lumumba na Ikulu jijini Dar es Salaam, kuwasikiliza.

Msimamo wa UKAWA uko wazi, tunataka maoni ya wananchi yaheshimiwe na Bunge Maalum la Katiba.

Mungu Ibariki Tanzania!

Imetolewa na;

-----------------------------------Freeman Alkael Mbowe(MB),Mwenyekiti - CHADEMA

--------------------------------------Ibrahim Haruna Lipumba(MBMK)Mwenyekiti – CUF – Chama Cha Wananchi,

--------------------------------------James Francis Mbatia(MB)Mwenyekiti – NCCR MAGEUZI.

Monday, March 24, 2014

AZAM FC, YOUNG AFRICANS, MBEYA CITY UBINGWA BADO KITENDAWILI: MASHABIKI

Na Samwel Mbugi, Mbeya.
Wadau na wapenzi wa soka jijini Mbeya wametoa maoni yao kuhusiana na msimu huu wa mashindano ya ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/2014 wakilinganisha na mashindano ya msimu wa mwaka jana 2012/2013.

Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti walisema kuwa msimu huu ni mgumu sana ikilinganishwa na miaka mingi iliyopita timu zilizo kuwa zinaonyesha upinzani mkubwa dhidi ya Young Africans Sports Club (Yanga) na Simba Sports Club zilikuwa chache lakini msimu huu unaonesha kila timu imejipanga kuleta ushindani mkali bila kuogopa vilabu vikongwe.

Pia walisema kuwa mwaka huu haitabiriki haraka timu itakayochukua ubingwa kwani kila timu inaonekana kujianda vyema kitu ambacho kimeleta changamoto kwa timu kubwa zilizozoea kuchukua ubingwa wa mashindano ya ligi kuu Tanzania Bara.
Mpaka sasa Timu za Azam FC, Young Africans Sports Club na Mbeya City zina nafasi kila moja ya kutwaa ubingwa mwaka huu.

Bingwa mtetesi Young Africans Sports Club yupo nyuma kwa pointi 4 dhidi ya makamu bingwa Azam FC mwenye pointi 47 na akiwa na mechi moja mkononi, huku Mbeya City akiwa na Pointi 42.
Kikosi cha  wachezaji wa Jangwani Young African Sports Club wakiwa katika picha ya pamoja. Timu ya Yanga ili kutetea ubingwa inatakiwa kushinda mechi zilizobaki huku ikiombea tinu ya Azam ikifungwa ama kutoa suluhu mechi zilizobaki. (Picha Kwa msaada wa tovuti ya Young Africans Sports Club)
Wachezaji wa Young Africans Sports Club wakicheza kiduku bada ya kufunga goli la Kuongoza dhidi ya Azam FC (Picha Kwa Msaada wa Full Shangwe)
Wachezaji wa Azam FC wakishangilia goli baada ya kurudisha goli dhidi ya Yanga mechi ambayo iliisha kwa timu hizo kufungana 1:1.(Picha Kwa Msaada wa Full Shangwe)
Sambamba na hayo wengi wao walitoa ponge kwa timu ya Mbeya City kwa kuonyesha upinzani mkubwa licha ya kuwa ni mara ya kwanza kucheza mashindano hayo ya ligi kuu Tanzania Bara.

Wamezitaka timu za ligi daraja la kwanza kuiga mfano kwa timu ya Mbeya city.
Wachezaji wa Mbeya City pamoja na mashabiki wao wakishangilia ushindi wa 2:0 dhidi ya Ruvu Stars. (Picha Kwa Msaada wa Full Shangwe)

Katiba mpya itapatikana kweli Tanganyika


Sunday, March 16, 2014

ASIYEKUBALI KUSHINDA SI MSHINDANI KALENGA, IRINGA

Akina mama mkoani Iringa katika Jimbo la Kalenga wakishangilia baada ya Godfrey Mgimwa kuibuka mshindi wa ubunge jimboni hapo
Uchaguzi wa jimbo la kalenga uwe fundisho kwa chaguzi zijazo kwa vyama vya siasa na vyombo vya dola vinavyohusika kulianda Amani na usalama wa nchi pamoja na raia wake.


Godfrey Mgimwa akinyanyuliwa na mmoja wa viongozi wa CCM mkoani Iringa katika Jimbo la Kalenga baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi ulifanyika Machi 16 mwaka huu akirithi kiti cha ubunge kilichoaachwa wazi na baba yake baada ya kufariki dunia.

Licha ya uchaguzi wa jimbo la Kalenga kumalizika na Godfrey Mgimwa (CCM) kuibuka kidedea bado umeacha kovu lisilotibika haraka miongoni mwa walioumizwa kipindi cha kampeni za uchaguzi huo.
Katika kampeni hizo CHADEMA na CCM vilikuwa vikituhumiana kwa kuwatumia vijana katika matukio ya kiuhalifu kama vile kuwakamata viongozi wa vyama hivyo na kuwapiga na hata kuwateka viongozi hao.
CCM waliwatuhumu wafuasi wa CHADEMA kupiga na kumuumiza kiongozi wa CCM na dereva wa Naibu Waziri wa Uchumi Mwigulu Nchemba wakati CHADEMA wakiwatuhumu wafuasi wa CCM kwa kumpiga mchungaji wa kanisa la Orthodox, na kumpiga mbunge wa viti maalum wa CHADEMA Rose kwa madai alikuwa anatoa rushwa kwa wapiga kura.

Kasoro zote zilizojitokeza kipindi cha kampeni hadi uchaguzi serikali na vyama vya siasa havina budi kutafuta suluhu ya kutatua kasoro hizo ikiwemo kuwafundisha vijana wao namna ya kufanya kampeni za Amani kwa kutoa sera za kuwashawishi wananchi wamkubali mgombea badala ya kushindana kwa virungu na mapanga.
Matukio haya yote kama yatafumbiwa macho hakika yataliingiza  taifa katika machafuko ya kisiasa yasiyo na tija yoyote kwa taifa hili.
Kukomaa kwa Demokrasia si kushindana kwa kupigana bali ni kushindana kwa sera na pindi mtu anaposhindwa katika uchaguzi baada ya wananchi kuamua kumpa kura mtu mwingine, aliyeshindwa basi anakubaliana na matokeo na kumpongeza aliyepita.
Sasa baada ya wanakalenga kumchugua Godfrey Mgimwa kuwa mbunge wao, mbunge huyo hana budi kuondoa tofauti zao zote na wanachama wa vyama vya upinzania na kuwatumikia wananchi wake kwa kuhakikisha ahadi zilizo ahidi katika kipindi hiki kifupi cha uchaguzi anazitekeleza kwa muda mwafaka ilikujiwekea mazingira ya kukubalika na wananchi wa kalenga.
Wanakalenga hawakuhitaji na wala hawakumchagua kwa ngonjera za ahadi bali wamempa fursa hiyo ya kuwatumikia wananchi hao baada ya kumwona ametambua matatizo wanayokabiliwa nayo ambayo mbunge huyo atayatatua katika kipindi hiki kifupi cha mwaka mmoja.
Hata hivyo si dhambi kwa mbunge mteule Mgimwa akatimiza baadhi ya malengo ambayo yaliaachwa na marehemu Williamu Mgimwa badala ya kuongeza ahadi nyingi zisizotekelezeka kwa wanakalenmga kwa lengo tu aonekana ana ahadi na malengo mazuri kwa wananchi wa Kalenga.
Aidha, katika kampeni wanafunzi ama watoto walichukuliwa kama mfano wa kuonesha namna gani serikali ya chama tawala inavyoshindwa kuwasaidia wananchi hata wanafunzi katika kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ya jamii.
Ni wazi sasa aliyepita atahakikisha pia wanafunzi waliooneshwa kama mfano wa wanafunzi wanaotoka katika familia masikini wanasaidie na wanapata elimu sawa na watoto wa vigogo badala ya kuwaacha watoto katika mazingira yale yale ambayo hayaoneshi utofauti wo wote wa chama hicho kugundua kuwa watoto hao wanatoka katika familia masikini.
Hata hivyo kuna haja ya kuangalia upya sheria ya vyama vya siasa ili ifanyiwe mabadiliko kutokana na sheria hiyo kutokuwa na kikomo cha idadi ya vyama vya siasa vinavyotakiwa kusajiliwa nchini.
Kutokana na sheria hiyo kukosa meno ya imesababisha utitiri wa vyama vingi vya siasa ambavyo vinaonekana kuanzishwa kwa malengo ya kupata ruzuku ambayo inaingia mifukoni mwa watu wachache.
Ruzuku zinazotolewa kwa vyama vya siasa ni fedha za wananchi ambazo zingeweza kuwasaidia wananchi katika mambo mengine ya msingi kwa jamii.

Uwingi wa vyama vingi nchini Tanzania haumanishi kukomaa kwa Demokrasia kwa kuwa nchi zilizoendelea kama marekani ina vyama viwili tu na bado ni nchi iliyokomaa kidemokrasia.
Wapiga kura katika Jimbo la Kalenga Mkoani Iringa wakiwa tayari kwa kupiga kura kumchagua mgombea wapendaye baada ya kampeni za kujinadi wagombea hao kuwashawishi wananchi hao na kuamua kwa hiari yao nani wape kura zao. (Picha kwa msaada wa Michuzi blogu)

Wednesday, March 12, 2014

ELIMU YA SIASA NA URAIA KWA VIJANA YAHITAJIKA TANZANIA



Imedai kuwa wimbi la vijana kujiingiza katika siasa limezidi kuwa kubwa huku wengi wao wakiwa na elimu duni ya siasa hali inayochangia wao kutumiwa vibaya na wanasiasa.
NGUVU YA HABARI imefanya mahojiano na viongozi wa umoja wa vijana chama cha wananchi -CUF, Baraza la Vijana la CHADEMA na wachambuzi wa masuala ya siasa ili kujua ni njia gani zinaweza kutumika ili kuhakikisha vijana wanapata elimu ya siasa kuondoka na kutumika vibaya katika mambo ya siasa.
Mwekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), John Heche amesema  CHADEMA kimekuwa kikitumia kila njia kuhakikisha vijana wapata elimu ya siasa na kuwapa fursa vijana kugombea ngazi mbalimbali za uongozi ili kueneza elimu kwa vijana wenzao.

BOFYA HAPA KUMSIKILIZA JOHN HECHE MWENYEKITI WA BAVICHA-CHADEMA………..
JOHN HECHE akiwa katika shughuli zake za kisiasa mbele ya waandishi wa habari

Naye katibu wa Umoja wa vijana  CUF, HAMIDU BOBALI amewataka wabunge wa katiba kupitisha  baraza la vijana la taifa ambalo litawaunganisha vijana kujadili mambo mbalimbali yanayowahusu ikiwemo elimu ya siasa.

Katika mahojiano  Mchambuzi wa maswala ya siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk. Benson Bana amesema vijana wengi wamekuwa wakitumika kisiasa visivyo kutokana na wengi wao kukosa elimu ya uraia.
BOFYA HAPA KUMSIKILIZA DK Bana……………… 
 
Naye mchambuzi wa masuala siasa Profesa Mwesigwa Baregu alipohojiwa kwa nyakati tofauti na NGUVU YA HABARI kuhusiana na uelewa wa vijana juu ya  itikadi za vyama vya siasa amesema kuna vijana wamekuwa wakijitahidi kujifunza masuala ya siasa na kufanya tafiti mbalimbali za vyama vya siasa zinazowasaidia kujua itikadi za vyama vyao na kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya kisiasa yanayoikumba jamii inayowazunguka.
Aidha Profesa Baregu amewataka baadhi ya vijana ambao wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kushabikia vyama ama wanasiasa bila kujua itikadi za vyama  kuachana na tabia hizo za ushabiki wa vyama vya sisiasa na badala yake wajifunze sera za vyama hivyo wanavyovipenda ili kuweza kuchambua ubora wa sera za vyama hivyo.
BOFYA HAPA KUMSIKILIZA Prof Baregu………………..
Prof. Baregu asisitiza elimu ya urai kwa vijana
Aidha profesa Baregu ameasa vyama vya siasa kutoa elimu ya siasa kwa vijana wao ili kuwawezesha  kujua imani, itikadi na sera za vyama vyao badala ya kuacha njiapanda wakielea bila kujua itikadio za vyama vyao,
Hata hivyo, vijana walipohojiwa kwa nyakati na NGUVU YA HABARI kutaka kujua nini kunawavutia kujiingiza katika masuala ya siasa kwa wingi zaidi na wana uelewa gani wa itikadi za vyama wanavyoshabikia, wamekuwa na majibu tofauti huku wengi wao wakisema ugumu wa maisha ndio unao wafanya wajiingize katika vyama vya siasa hata kama hawaelewi hatima ya maisha yao.
VIJANA WANASEMAJE............