NGUVU YA HABARI

Friday, January 17, 2014

Kiza cha Tandaa Uhuru wa Vyombo vya Habari Tanzania

TAKRIBANI miaka hamsini na miwili imepita toka Tanzania Bara ipate Uhuru wa kisiasa. Watanzania wengi wamekuwa wakifurahia Uhuru huo huku waandishi wa Habari wakiendelea na harakati za kutafuta Uhuru wa vyombo vya habari licha ya wakoloni kuwaachia Uhuru wa kisiasa watanzania toka mwaka 1961 Disemba 9.
Kutoka na kukosekana kwa Uhuru wa vyombo vya Habari nchini, watanzania wameshuhudia kufungiwa kwa vyombo vya Habari kama vile kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi mwaka 2008 miezi mitatu, na Julai 30 mwaka 2012 limefungiwa kwa muda usiofahamika, kuuawa kwa mwandishi wa Habari Daud Mwangosi, na kutekwa na kuteswa kwa Absalum Kibanda, kutishiwa kwa waandishi wa habari.


Waandishi wa habari wakiwa katika harakati za kuhakikisha wanapata picha za chanzo chao cha habari na baadaye kuandaa habari hiyo kwa manufaa ya msikilizaji au mtazamaji.


Maandamano ya Waandishi wa habari wa Nigeria wakipinga ukandamiza wa uhuru wa vyombo vya habari nchini humo.

Waandishi wa habari wakiendeleza maandamano ya kupinga mauaji kwa waandishi wa habari yanayodaiwa kufanywa na vyombo vya usalama wa raia. (Picha imechukuliwa Mtandaoni)

Kilio cha waandishi wa Habari Tanzania ni matokeo yaliyosababishwa na serikali ya wazawa kurithi sheria iliyotungwa na Bunge la serikali ya kikoloni la Tanganyika ambalo liliundwa mwaka 1926 na mwaka 1928, bunge hilo la Tanganyika lilitunga Sheria ya Magazeti Na. 22 ya mwaka 1928 kuzuia machapisho yoyote yaliyokuwa yakipinga utawala wa serikali ya kikoloni na kuwataka wananchi wawaunge mkono wanaharakati wa Uhuru.
 Serikali ya kikoloni ya Waingereza ilitunga sharia hiyo ilikudhibiti makundi ya wanaharakati waliokuwa wakitumia vyombo vya Habari kupinga na kukosoa utawala wa kikoloni na ambao pia walikuwa wakipigania Uhuru wa mwaafrika kujitawala mwenyewe.
Aidha, Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) Dk. Ayub Rioba katika kitabu chake cha ‘Historia ya Vyombo vya Habari Tanzania’ (The Media History of Tanzania) aliandika kuwa mwaka 1952 Agosti Bunge la Tanganyika lilikaa kikao na kufanyia marekebisho ya Sheria ya Magazeti Na. 35 ya 1952 ambapo vifungu vya jinai  za kashfa na uchochezi vilipitishwa na bunge hilo na lilipendekeza adhabu kwa mwandishi wa Habari atakayekiuka vifungo hivyo kulipa faini ya Dola za Marekani $ 400 hadi $ 1300.
Muathirika wa kwanza wa sharia hiyo alikuwa Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tanganyika African Nation Union (TANU) pamoja na wenzake walikamatwa kwa madai waliandika Habari za uchochezi.
Kukamatwa kwa Mwalimu Nyerere na wenzake kulichochea zaidi waandishi wa Habari kuichukia serikali hiyo kwa madai inatumia sheria kandamizi kuzuia harakati za ukombozi wa Mtanzania kutoka mikononi mwa Waingereza.
Kila lililo na mwanzo halikusikuwa na mwisho, hatimaye Tanganyika ikapata Uhuru wake Disemba 9, mwaaka 1961, na Zanzibar kufanya Mapinduzi tarehe 12 Januari 1964 na kisha mwaka 1964, Aprili 26, Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hali hiyo ilidhaniwa ingepoteza machungu ya waandishi wa Habari kunyanyaswa na wakoloni.
Pema ukipema si pema tena, baada ya Muungano wa za Tanganyika na Zanzibar Uhuru mwandishi wa Habari ukabaki kitendawaili pale Serikali ya wazawa iliyokuwa ikitumia magazeti na redio kuhubiri harakati za ukombozi wa mwafrika na ujenzi wa taifa jipya mwaka 1976 ikatunga sheria ya Magazeti Namba 3 na kusainiwa na Rais Mwalimu Nyerere April 3, 1976 ambayo ikaendeleza kiama cha kumnyimwa uhuru mwaandsishi wa Habari na kumfanya aendelee kukumbuka machungu ya wakoloni.
Aidha, sheria hiyo iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo sheria iliyokuwa ikipingwa vikali na wanaharaki hao wakati wa kupigania Uhuru wa mwaafrika kipindi cha ukoloni na baada ya kupata Uhuru sheria hiyo ilirithiwa tena bila kujali kama ni sheria ile ile iliyomweka hatiani Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Mbali ya sharia hiyo kandamizi ya Magazeti ya mwaka 1976, mwandishi wa Habari amejikuta akishindwa kufanya kazi ya kuutumikia umma kupitia vyombo vya Habari kutokana na kuwepo pia sheria nyingine zinazombana.
Sheria ya Usalama wa Taifa (National Security Act No. 6 of 1970) iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungana 19 Machi 1970 ni mojawapo ya sheria zinazobinya Uhuru wa mwandishi wa Habari kwa kuzuia mambo ambayo yanadaiwa kuwa nyaraka za siri za taifa amabazo hazitakiwi kuandikwa. Lakini nyaraka hizo hazijakuwekwa bayana zipi ni nyaraka za siri na zipi si nyaraka za siri hasa kipindi hiki ambacho serikali inasisitiza utawala bora na uwazi.
Wakati wa waandishi wa Habari wakitafuta namna ya kujikomboa mikononi mwa adui wao wa Uhuru wa vyombo vya Habari, kiza kilizidi kutawala kwa wanahabari na wadau wa Habari pale serikali ilipopeleka muswada wa marekebisho ya sheria ya habari bungeni ikiwa imejaa vipengee vinavyozidi kuwakandamiza waandishi wa habari na vyombo vya Habari kwa kupendekeza adhabu ya sh milioni tano au kifungo cha miaka mitano au vyote kwa pamoja.
Hata hivyo muswada huo wa marekebisho ya sheria ya magazeti ya mwaka 1976 sura ya 229 Bunge uliyokuwa na lengo la kuwatia kitanzi waandishi wa habari na vyombo vya Habari vitakavyochapisha habari zilizodaiwa za uvunjivu wa amani au uchochezi ulipingwa bungeni Novemba 8 mwaka jana na huku wabunge wengi waliitaka serikali kufanya mabadiliko kamili ya sheria ya habari.
Kilio cha waandishi wa Habari kilioneka kuungwa mkono pale spika wa Bunge Anne Simamba Makinda aliposema anaishangaa serikali kuona ikiendelea kuweka viraka vya sheria ya magazeti badala ya kuipeleka bungeni ifanyiwe mabadiliko yote.
“Tumefanya utani katika sheria hii kwa muda mrefu, sitaki utani. Serikali leteni muswada wa sharia ya Habari,” alisisitiza Spika wa Bunge Makinda.
 Kuendelea kutumia sheria zinazoingilia Uhuru wa vyombo vya Habari ni sawa na kuenzi utawala wa kikoloni ambalo ulitunga sheria za kubinya Uhuru wa vyombo vya Habari katika kuikosoa serikali ili kuzidi kuwapumbaza wananchi wasitambue kama wanaibiwa haki na maliasili zao, wananyonywa, wananyanyaswa na kubaguliwa na serikali ya kikoloni.
Aidha, kuwepo kwa sheria zinazonyima Uhuru wa waandishi wa Habari zinachangia pia kurudisha nyuma Maendeleo ya nchi kwa kuwa Uhuru huendana na Maendeleo.

Waandishi wa habari wakimsikiliza Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe akitolea ufafanuzi wa kuvuliwa nyadhifa zake na kamati kuu ya CHADEMA kwa tuhuma za kukihujumu CHADEMA
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika kitabu chake cha ‘Uhuru na Maendeleo’ alisema; “Uhuru na Maendeleo ni vitu vinavyohusiana sana; uhusiano wao ni sawa na uhusiano baina ya kuku na yai! Bila kuku hupati mayai; na bila mayai kuku watakwisha. Vilevile bila ya Uhuru hupati Maendeleo, na bila ya Maendeleo ni dhahiri Kwamba Uhuru wako utapotea.”
Ili Tanzania itimize azma ya kuwa na maendeleo ya uchumi, kisiasa na kijamii inahitaji kufanya mabadiliko makubwa katika sheria zinazonyima Uhuru wa mwandishi wa Habari ili kutoa fursa kwa waandishi wa Habari kufanya Habari za uchunguzi na upembuzi yakinifu ambao pia utasaidia kuwaunganisha wananchi na serikali yao katika kupanga na kutekeleza mambo yanayowahusu.
Vilevile kuwapa Uhuru waandishi wa Habari kwa kuondoa sheria kandamizi kutawapa nafasi waandishi wa Habari kufichua mambo mbalimbali ambayo ni kikwazo cha maandeleo ukiwemo ufisadi rushwa na mikataba ya ulaghai inayoiingizia hasara taifa.
Kutokana na kuwepo kwa nyaraka nyingi za siri kulipelekea gazeti la Mwananchi kufungiwa wiki mbili baada ya kuchapisha taarifa za mishahara ya watumishi wa umma ambayo wanalipwa na kutokana na kodi ya wananchi.
Baba wa taifa katika kitabu chake cha ‘Uhuru na Maendeleo alisema, “Utumiaji wa nguvu, na kutoa ahadi za uwongo, mambo hayo yanaweza kuleta mafanikio kwa muda mfupi tu. Hayawezi kuleta nguvu kwa taifa au kijiji, wala hayawezi kuweka msingi wa Uhuru wa watu, au usalama wa mtu binafsi au wa kikundi cha watu.
Iwapo serikali itasikia kilio cha waandishi wa Habari wanaopinga sheria kandamizi basi mchango wa vyombo vya Habari katika Maendeleo ya nchi utaonekana kwa uwazi.

Toka sheria ya Magazeti itungwe mwaka 1976 na kusaini na Baba  wa taifa na rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Nyerere tarehe 3, Aprili 1976 ni takribani miaka 38 imepita serikali haijawahi kupeleka muswada wa Habari bungeni.


Umoja wa Waandishi wa Habari mkoani Mbeya wakilaani mauaji kwa waandishi wa habari pamoja na vitisho wanavyotishiwa na vyombo vya usalama mara baada ya mwandishi wa Habari Daud Mwangosi kuuawa katika kijiji cha Nyololo Wilayani Mufindi-Iringa Septemba 2, 2012. (Picha imechukuliwa Mbeya Yetu Blog)

Ahadi Hewa kwa Wananchi za Nini?

KILA mbunge ana wajibu wa kusikiliza kero za wapiga kura wake na kuziwasilisha kezo hizo serikalini zipatiwe ufumbuzi pamoja na kusimamia shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika jimbo lake.
Ili kuwakilisha kero hizo zinazowasibu wapiga kura, wabunge mara nyingi hutumia vikao vya bunge kufikisha kero za wananchi kwa serikali ambapo majibu hutolewa papo kwa hapo ama serikali huomba ipewe muda kuangalia uwezakano wa kutafuta majibu ya ufumbuzi wa kezo za wananchi wake.
Wananchi wanaposikia mbunge wao anahoji maswali bungeni kuhusiana na utatuzi wa kero zao hutega masikio kwa makini ili kutaka kupata majibu na hufurahi zaidi pale serikali inapotoa majibu kuwa tatizo hili limepokelewa na litatatuliwa na kubaki historia baada ya muda fulani.
Lakini majibu hayo yanayojibiwa na  serikali kupitia  mawaziri wa wizara husika mbungeni yamekuwa ya kuwatia moyo wananchi na baada ya vikao vya bunge kumalizika na bunge kuahirisha mkutano wake, utekelezajia wa kero hizo hususua halia ambayo huiongeza maswali ya ziada jamii inayokerwa na matatizo hayo.
Mfano, tatizo la maji limekuwa kero Tanzania nzima, serikali imekuwa ikitoa ahadi za ufumbuzi wa tatizo hili kwa kujinadi kuwa italitatua tatizo na kubakia historia tu ya tatizo.
Vijana kwa wazee wakichomwa na mionzi ya jua bila kujali athari za mionzi ya jua hilo ili mradi wao wapate nafasi ya kuteka maji. Uhaba wa maji nchini Tanzania bado ni kitendawili ambacho hakipatiwa jibu. (Picha imechukuliwa mtandaoni)
Mwaka 2012, Juni 22, Mbunge wa Mufindi Kusini, Menrad Kigola (CCM),  alihoji ni kwa nini serikali isifanye ukarabati wa matanki ya maji ambayo ni mabovu katika vijiji vya Sawala, Nyololo, Maduma, Nyigo, Kibao na Igowole ili yaweze kutumika pamoja na kutaka kujua ni lini serikali itaanza ukarabati wa miundombinu ya maji ya mto Nzivi ili kuwezesha wananchi wa vijiji jirani kupata maji ya uhakika.
Serikali kupitia kwa Naibu waziri Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), AGGREY MWANRI, alisema Serikali imeweka mikakati katika kuhakikisha mpango wa maji unaanza mara moja kufanya kazi ya kuhudumia vijiji vya malamaziwa, Maguvani, Iramba, ukemele, Nyanyembe, Kinegembasi na Idetero.
Naibu waziri ofisi ya tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), AGGREY MWANRI alisema Serikali imeweka mikakati katika kuhakikisha mpango wa maji unaanza mara moja kufanya kazi ya kuhudumia vijiji vya Mbalamaziwa, Maguvani, Iramba, Ukemele, Nyanyembe,Kinegembasi na Idetero.
Aidha, Serikali ilikiri kutambua ubovu wa matanki hayo na kusema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13 serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 804.1 kwa ajili ya kazi hiyo ya ukarabati wa matanki hayo kwa kununua mabomba mapya.
 “kwa kutambua umuhimu huo, halmashauri katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13 imetenga sh bilioni 804.1 kwa ajili ya kazi hiyo ambapo itafanya kazi ya ukarabati wa banio, kuweka mabomba mapya na kuimarisha mifumo yote ya maji,” alisema Mwanri.
Majibu hayo ya serikali yaliwafariji wananchi ambao walikuwa wakimsikiliza kwa umakini naibu waziri ofisi ya tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI  akijibu bungeni kupitia vyombo vya habari vilivyokuwa vinarusha matangazo ya vikao vya bunge na wafurahia kuwa tatizo lao serikali imelivalia njuga kulimaliza katika mwaka wa fedha 2012/2013.
Pamoja na majibu mazuri ya serikali, utekeleza huo wa ukarabati wa matanki ya Nyololo, Maduma, Igowole, Sawala, Nyigo na Kibao na ambao ulitengewa bajeti ya mwaka 2012/2013 haujafanyika mpaka sasa, huku baadhi ya matanki kama tanki la maji la Maduma likendelea kuvuja maji kwa sababu ya uchakavu wa miundombinu yake.
Swali  la kujiuliza kwa nini ukarabati wa matanki hayo hujafanyika hadi sasa wakati serikali iliahidi kuwa tayari imeshaanda fedha shilingi bilioni 804.1 kwa ajili ya mradi huo wa maji? Wananchi wamlaumi nani kwa kuendelea kuhangaika kwa uhaba wa maji sasa na wale ambao hawana matanki?
Hivi, ni kweli serikali ilitoa majibu katika kikao cha bunge ili kufariji tu wananchi lakini ilikuwa haijaandaa fedha hiyo katika mwaka wa fedha 2012/201? Kwa kuwa bajeti ya mwaka 2012/2013 iliisha toka bunge lilipopitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014.
Mbunge wa Mufindi kusini, Menrad Kigola alipohojiwa  ili kutoa ufafanuzi juu ya kusuasua ukarabati wa matanki mabovu ya vijiji hivyo, alisema hakuna ukarabati ambao serikali imekwisha kuufanya toka itoe ahadi ya ukarabati huo.
Mbunge Kigola alidai serikali ilijichanganya kujibu kwa kuwa kulikuwa hakuna bajeti ambayo ilitengwa kwa ajili ya ukarabati wa matanki mabovu na mradi wa maji wa mto nzivi isipokuwa kulikuwa na fedha zilizotolewa na benki ya Dunia kwa ajili ya uchimbaji visima vya maji.
“Naibu waziri alijichanganya tu kujibu, yalikuwa ni makosa tu ya kibinadamu kusema serikali imetenga bajeti ya shilingi bilioni 804.1/= kwa ajili ya mradi huo wa maji,” alisema Mbunge Kigola.
Swali la kujiuliza, je wananchi wanakuwa na imani gani kwa serikali yao ambayo iliwaahidi kuwaondolea kero ya maji kwa kufanya ukarabati wa matanki hayo, lakini hadi sasa haijatekeleza bila kutolea maelezo kuwa naibu waziri alijichangaji kujibu tu, ukweli hakukuwa na bajeti hiyo?
Kukaa kimya kwa serikali kuna maanisha nini kwa wananchi wake ambao wamekuwa wakisikiliza majibu na ahadi zinazotolewa na serikali bila kutekelezwa? Je, hili nalo serikali inasubiri mwongozo ili ipate nafasi ya kukiri kukosea?
Hivi serikali haina utaratibu wa kukagua utekelezaji wa kero za wananchi ambazo imepokea kupitia wawakilishi wao katika vikao vya bunge kama zimetekelezwa au la? Badala ya utekelezaji kubakia kwenye maandishi huku wananchi wakiendelea kuonja uchungu wa maisha.
Na kama serikali inatuma mapema fedha hizo za mradi na halmashauri zinashindwa kutekeleza kwa nini serikasli isiwachukulie hatua wanachelesha shughuli za kimaendeleo?
Mwanakijiji akichota maji kisimani bila kujali kama ni maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu hii ni kwa sababu ya uhaba wa maji katika maeneo mengi nchini Tanzania. (Picha imekuchuliwa mtandaoni)
Hali hii ya serikali kutoa majibu ya faraja bungeni bila utekelezaji kuna rudisha nyuma shughuli za kimaendeleo na kupoteza imani kwa wananchi.
Aidha, wabunge wametumwa kuwawakilisha wananchi kuhakikisha wanaishauri na kuikumbusha serikali inaposahau kutekeleza ahadi na wajibu wake wakutatua matatizo ya wapiga kura bila wabunge kusubiri wananchi wawakumbushe kuhusiana na miradi iliyoahidi na serika kuwa haijatekelezwa.
Ili serikali iepuke lawama hizo kwa wananchi haina budi kuhakikisha ahadi zinazotolewa zinatekelezwa kwa wakati.

Wabunge wakiwa bungeni mjini Dodoma ambako wabunge hukaa na kuishauri serikali, kutunga sheria pamoja na kuwasilisha kero za wapiga kura wake kwa serikali ilizipatiwe utatuzi