Na Nazael Mkiramweni, Dodoma
Wakazi wa mkoa
wa Dodoma wamemwomba Rais John Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza kwenye
ofisi za Mamlaka ya ustawishaji makao makuu (CDA) ili kujionea uonevu
unaofanywa na mamlaka hiyo.
Walisema kuwa
moja ya uovu ni katika kuwanyang’anya wananchi ardhi yao bila kuwalipa
fidia.
Ombi hilo
limetolewa na wananchi hao wakati wakimpongeza Rais Magufuli kwa utendaji wake
wa kazi ndani ya siku 30 alizokaa ikulu.
Akizungumza kwa
niaba ya wenzake Chifu Lazaro Chihoma alisema kuwa wakazi wa Manispaa ya Dodoma
wana mategemeo makubwa na Rais Magufuli ya kuwasaidia ili waweze kupata ardhi
ambayo wanaililia kwa muda mrefu bila mafanikio.
Alisema
wafanyakazi wa CDA walipokuwa wanaanza kazi hawakuwa na usafiri hata wa
baiskeli lakini ndni ya kipindi kifupi tu wameanza kuendesha magari ya gharama
kubwa huku wakimiliki viwanja zaidi ya kumi huku wananchi wakiwa hawana viwanja
hata vya kujenga nyumba.
Naye Annarose
Ngallya mkazi wa Kata ya Dodoma Makulu alimwomba Dk, Magufuli kuiangalia kwa
jicho la huruma kata hiyo kwa kuwa ndiyo pekee ambayo wakazi wake hawajui hatma
yao kufuatia CDA kutowapimia ardhi ya kujenga.
Wakazi hao
walisema endapo Rais magufuli hataingilia kati suala la mgogoro wa ardhi kati
yao na CDA azma yake ya kuwapatia Wtanzania maisha bora haitafikiwa.
Naye Mussa
Mloha ambaye ni mlemavu wa macho alisema kuwa itakuwa vyema kama Rais
Magufuli atafika mkoani Dodoma kukagua idara mbalimbali kwa nako hali si shwari.