NGUVU YA HABARI

Tuesday, December 8, 2015

Wakazi Dodoma: Magufuli uko wapi?



Na Nazael Mkiramweni, Dodoma

Wakazi wa mkoa wa Dodoma wamemwomba Rais John Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Mamlaka ya ustawishaji makao makuu (CDA) ili kujionea uonevu unaofanywa na mamlaka hiyo.

Walisema kuwa  moja ya uovu ni katika kuwanyang’anya wananchi ardhi yao bila kuwalipa fidia.

Ombi hilo limetolewa na wananchi hao wakati wakimpongeza Rais Magufuli kwa utendaji wake wa kazi ndani ya siku 30 alizokaa ikulu.
 Akizungumza kwa niaba ya wenzake Chifu Lazaro Chihoma alisema kuwa wakazi wa Manispaa ya Dodoma wana mategemeo makubwa na Rais Magufuli ya kuwasaidia ili waweze kupata ardhi ambayo wanaililia kwa muda mrefu bila mafanikio.
Alisema wafanyakazi wa CDA walipokuwa wanaanza kazi hawakuwa na usafiri hata wa baiskeli lakini ndni ya kipindi kifupi tu wameanza kuendesha magari ya gharama kubwa huku wakimiliki viwanja zaidi ya kumi huku wananchi wakiwa hawana viwanja hata vya kujenga nyumba.

 Naye Annarose Ngallya mkazi wa Kata ya Dodoma Makulu alimwomba Dk, Magufuli kuiangalia kwa jicho la huruma kata hiyo kwa kuwa ndiyo pekee ambayo wakazi wake hawajui hatma yao kufuatia CDA kutowapimia ardhi ya kujenga.

 Wakazi hao walisema endapo Rais magufuli hataingilia kati suala la mgogoro wa ardhi kati yao na CDA azma yake ya kuwapatia Wtanzania maisha bora haitafikiwa.

Naye Mussa Mloha ambaye ni mlemavu wa macho alisema kuwa itakuwa vyema kama Rais Magufuli atafika mkoani Dodoma kukagua idara mbalimbali kwa nako hali si shwari.

No comments: