NGUVU YA HABARI

Tuesday, December 8, 2015

Pius Mzimbe: Boresheni Miundombinu



Serikali imetakiwa kuboresha miundombinu ya barabara zinazoingia katika hifadhi za taifa ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea hifadhi hizo.

Rai hiyo imetolewa na Mhifadhi mkuu wa hifadhi ya taifa ya Kitulo iliyopo kati ya mkoa wa Mbeya na mkoa wa Njombe Pius Mzimbe wakati akizungumza na waandishi wa habari za Utalii na uwekezaji nchini(TAJATI) waliofanya ziara ya siku moja katika hifadhi hiyo chini ya ufadhili wa shirika la Wildlife Conservation Society(WCS).

Mzimbe amesema kuwa kumekuwa na idadi ndogo ya watalii wa ndani na pamoja na wa nje wanaofika kujionea vivutio vinavyo patikana katika hifadhi ya Kitulo kutokana na miundombinu ya Barabara kuwa mibovu.

Amesema iwapo kipande cha Barabara kutoka Chimala hadi Matamba chenye urefu wa kilomita 26 kitakuwa chini ya Wakala wa Barabara Tanroads itasaidia kuimarisha na kurahisisha watalii kufika kiurahisi  ndani ya hifadhi hiyo kuliko hivi sasa ambapo wengine wa watalii kurudia njiani hali ambayo huchangia serikali kukosa mapato.

Hifadhi ya Kitulo ilianzishwa mwaka 2005 lengo likiwa ni kutunza mandhari ya kipekee na makazi ya viumbe hai, kulinda vyanzo vya maji ya Mto Ruaha na Ziwa Nyasa na ni hifadhi ambayo ina vivutio ambavyo havipatikani katika hifadhi yoyote lakini pamoja na hayo imekosa watalii wa kutosha kutokana na miundombinu ya barabara inayokwenda katika hifadhi hiyo kuwa mibovu ambapo kwa mwaka hutembelewa na watali wasiozidi 700.


No comments: