Josea Sinkala, Mbeya
Baadhi ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika
shule ya msingi Ilomba iliyopo kata ya Isyesye jijini Mbeya wameilaumu kamati
ya shule hiyo kwa kutowapatia risiti za michango wanayochangia kwaajili ya
ujenzi wa shule hiyo.
Wamesema hali hiyo inawanyong’onyeza kuendelea
kuchangia kutokana na kutokuwa na uhakika wa michango yao kama inatumika kwa
lengo lililokusudiwa.
Wakizungumza katika kikao cha wazazi wamesema wameshangazwa
na kitendo cha kamati ya shule kushindwa kuwapatia risiti tangu michango hiyo
ianze kuchangishwa mwaka jana, hali inayosababisha wazazi hao kupata mashaka na
uongozi unaoshughulikia fedha hizo.
Hata hivyo kupitia mkutano huo, baadhi ya wazazi
wametoa kero zao juu ya walimu kuwarudisha wanafunzi nyumbani wakati wa masomo
na kuwatuma kufanya kazi za kilimo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo
Ezekiel Mwanzonje akizungumza na blogu ya Nguvu ya Habari baada ya
mkutano huo amekiri kuwepo kwa changamoto ya ugawaji risiti kufuatia baadhi ya
wazazi kutoa michango yao nusunusu hivyo amesema inawawia vigumu kutoa risiti
kwa wote.
Naye Mjumbe aliyekuwa akipokea michango Agness
Nyenze amesema pia tatizo linguine lililochangia wazazi kutopewa risiti zao kwa
wakati ni kutokana na kuchelewa kupewa kitabu cha risiti kutoka katika uongozi
wa kata.
Shule ya msingi Ilomba ilianzishwa zaidi ya miaka
sitini iliyopita ambapo mpaka sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
uhaba wa vyumba vya madarasa, ofisi na vyoo vya walimu na blogu ya Nguvu ya Habari imeshuhudia kuwepo kwa tundu moja la choo
linalotumiwa na walimu wote wa kike na kiume ishirini katika shule hiyo.
No comments:
Post a Comment